Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limesema umri wa kuishi barani Afrika kwa mtu mwenye afya bora, umeongezeka kwa wastani wa miaka 10 kwa mtu mmoja kati ya mwaka 2000 na 2019, ikiwa ni ongezeko la kubwa kuliko ukanda mwingine duniani, katika kipindi hicho kutokana na kuimarika kwa huduma za mama na mtoto.
Taarifa ya WHO, kanda ya Afrika iliyotolewa leo Agosti 5, 2022 jijini Brazaville Jamhuri ya Congo, imenukuu ripoti ya mwaka huu ya kufuatilia huduma ya afya kwa wote kanda ya Afrika, ripoti ambayo imetambua kuwa COVID-19 inaweza kutibua mafanikio hayo.
Ripoti hiyo imesema, “Tmebaini kuwa idadi ya miaka ambayo mtu anaishi akiwa na afya njema imeongezeka hadi umri wa miaka 56 mwaka 2019 kutoka umri wa miaka 46 mwaka 2000, ingawa bado tuko nyuma ya wastani wa Dunia wa umri wa kuishi wa miaka 64, na wastani wa kuishi duniani uliongezeka kwa miaka mitano pekee.”
Imesema kuwa, kuimarika kwa huduma za msingi za afya, mafanikio katika afya ya uzazi hasa kwa wajawazito, watoto wachanga na afya yam toto na maendeleo mazuri katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kama vile UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria ni moja ya sababu.
“Kwa wastani, utoaji wa huduma ya afya kwa wote, imeongezeka kutoka asilimia 24 mwaka 2000 hadi asilimia 46 mwaka 2019,” imesema taarifa hiyo.
Mafanikio hayo pia yanagusa kuzuia na kutibu magonjwa ya kuambukiza lakini ingawa mafanikio hayo yalitiwa kiza na ongezeko la ghafla la magonjwa kama vile moyo, kisukari na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza na ukosefu wa huduma za afya zinazolenga magonjwa hayo.
Akizungumzia ongezeko la umri wa kuishi Afrika, Mkurugenzi WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema ni ushahidi ya harakati za bara hilo kuboresha afya na ustawi wa wakazi wake kutokana na watu wengi kuishi maisha yenye afya.
Hata hivyo, ameonya kuwa maendeleo hayo yanatakiwa kuwa endelevu, kwani inahitajika hatua za kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile saratani au kansa, mafanikio yaliyopatikana yatatokomea.