Umoja wa Mataifa (UN) umeunga mkono ahadi na mipango ya Serikali ya Zimbabwe kufanya uchaguzi huru na haki Mwezi Julai mwaka huu.
Uchaguzi huo ambao bado haujapangiwa tarehe utakuwa uchaguzi mkuu wa kwanza katika historia ya nchi hiyo kufanyika bila kuwa na jina la Robert Mugabe ambaye nafasi yake imechukuliwa na Rais Emmerson Mnangagwa.
Tamko lililotolewa na Mtawala katika Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, Achim Steiner Jumapili hii imeeleza kuwa uchaguzi ni ufunguo muhimu katika maono ya taifa hivyo wataiunga mkono Zimbabwe.
“Kwa kuzingatia kwamba uchaguzi huu ni wa kwanza na muhimu kwa Wazimbabwe, Steiner anaunga mkono ahadi ya Rais Mnangagwa kuwa na uchaguzi huru wa haki na amani ambao utakuwa ni hatua nzuri katika kipindi hiki cha kubadili uongozi,” imeeleza.
Imeongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaahidi kutoa ushirikiano katika maandalizi ya uchaguzi huo pamoja na hatua za kuimarisha uchumi.
Rais Mnangagwa anatarajia kugombea kwa tiketi ya chama tawala cha Zanu-PF huku akitarajiwa kupata upinzani kutoka kwenye chama kipya cha siasa kilichosajiliwa hivi karibuni ambacho kinaungwa mkono na rais wa zamani, Robert Mugabe.