Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS umeelezea masikitiko yake kutokana na vitendo vya uporaji wa mifugo vinavyoambatana na mauaji ya raia na utekaji nyara katika jimbo la Equatoria Mashariki nchini humo.
Hayo yameelezwa na msemaji wa Umoja wa Mataifa (UN), Stephane Dujarric wakati akizungumza na waandishi wa habari hii leo Julai 16, 2022 jijini New York, nchini Marekani.
Mjumbe huyo, ameinukuu UNMISS ikisema kuwa tayari imepeleka walinda amani wa Umoja wa Mataifa eneo hilo, ili kuendesha doria ya masafa marefu ya siku nne kama njia ya kutokomeza ghasia na kurejesha Imani ya usalama miongoni mwa wanajamii.
“UNMISS inaendelea kuwepo kwenye eneo hilo na kushirikiana na mamlaka husika za maenoe hayo pamoja na jamii zilizoathirika ili kutathmini kwa kina kilichotokea na kisha kuepusha mashambulizi ya kulipiza kisasi,” amesema Dujarric.
Kwa mujibu wa Dujarric, hofu kubwa ya UNMISS inatokana na baadhi ya vijana wanaojipanga na kuhamasishana kufanya kampeni ya mashambulizi ya kurejesha mifugo yao iliyoibwa.
UNMISS inasema inaiomba serikali ya kitaifa Sudan Kusini, Serikali ya jimbo na Viongozi wa kijamii kuchukua hatua za dharura ili kuepusha kusambaa kwa ghasia zinazoweza kujitokeza.