Mratibu wa Misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi ya Palestina, Lynn Hastings amesema ana wasiwasi kuhusu ongezeko la ghasia katika baadhi ya maeneo ya Gaza na Israel.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa akiwa Jerusalem, Hastings amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la ghasia zinazoendelea ndani na karibu na mji wa Gaza kati ya wanamgambo wa Kipalestina na Israel.
“Ghasia hizo hadi sasa zimegharimu maisha ya Wapalestina 13 kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel, akiwemo mtoto wa miaka mitano na mwanamke mmoja na ripoti zinaonyesha kuwa zaidi ya Wapalestina 100 na Waisrael 7 wamejeruhiwa,” amebainisha Hasting.
Maeneo mengi ya makazi katika maeneo ya Gaza na Israel, yameshambuliwa na nyumba kuharibiwa, huku familia 31 zikiwa tayari zimeachwa bila makazi ambapo pia ameeelezea kuwa hali ya kibinadamu huko Gaza ni mbaya kutokana na ghasia zinazoendelea.
“Uhasama huu lazima usitishwe ili kuepusha vifo na majeraha zaidi ya raia huko Gaza na Israel. Kanuni na sheria za kimataifa za kibinadamu zikiwemo zile za kuchukua tahadhari na kuwa na uwiano lazima ziheshimiwe na pande zote.” Amesema mratibu huyo wa Misaada wa UN.