Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameelezea kusikitishwa kwake na idadi kubwa ya Wapalestina, wakiwemo watoto, waliouawa na kujeruhiwa kutokana na uhasama unaoendelea kati ya Israel na makundi ya wapalestina wenye silaha huko Gaza.
Taarifa iliyotolewa leo Agosti 12, 2022 jijini Geneva, Uswisi imemnkuu Bachelet akieleza takwimu kuwa wiki iliyopita, watoto 19 wa Kipalestina waliuawa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kupelekea idadi hiyo ya vifo tangu kuanza kwa mwaka hadi 37.
Amesema, “Watoto kumi na saba waliuawa wakati wa mapigano ya Gaza kuanzia tarehe 5-7 Agosti, na wengine wawili waliuawa mnamo Agosti 9 na kuumiza mtoto yeyote wakati wa vita kunasumbua sana, na mauaji na ulemavu wa watoto wengi mwaka huu ni jambo lisiloeleweka.”
Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, imethibitisha kuwa kati ya Wapalestina 48 waliouawa, kulikuwa na raia wasiopungua 22 wakiwemo watoto 17 na wanawake wanne na wengine 22 bado haijabainishwa jinsia na umri wao.
Kati ya Wapalestina 360 walioripotiwa kujeruhiwa, karibuni theluthi mbili walikuwa raia, wakiwemo watoto 151, wanawake 58 na wazee 19 katika matukio kadhaa, ambapo watoto waliainishwa kuwa ni wengi walio na majeraha.
Mashambulio kadhaa ya Israeli yalilipua maeneo ya kiraia na kusababisha vifo na uharibifu wa mali za raia, huku Kamishna Mkuu huyo akitoa wito wa uchunguzi wa haraka, huru, usio na upendeleo, wa kina na wa uwazi kufanyika katika matukio yote yaliyoripotiwa.