Umoja wa Ulaya umetangaza utaratibu mpya kwa ajili ya kudhibiti mauzo ya chanjo za corona. Kulingana na taratibu hizo nchi za Umoja wa Ulaya zitakuwa na mamlaka ya kuzuia uuzaji wa chanjo hizo nje ya jumuiya hiyo.
Taratibu hizo kali zinaweza kuathiri usafirishaji kwa mataifa kama Uingereza, hatua ambayo inaonekana kuuongeza mzozo kati ya Jumuia ya Ulaya na nchi hiyo kutokana na uhaba wa chanjo hizo za kuokoa maisha
Ireland Kaskazini na Uingereza tayari zimeonesha wasiwasi kutokana na hatua hiyo, Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson walifanya mazungumzo kwa njia ya simu wakati ambapo waziri mkuu wa Uingereza alielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya athari inayoweza kutokea.
Aidha Shirika la afya duniani WHO limeikosoa hatua hiyo lakini Umoja wa Ulaya umeeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha kwamba kampuni za madawa zinatekeleza mikataba iliyosainiwa.