Katika safari ya mafanikio, ni kawaida kwa kila binadamu kukutana na mitihani. Wakati mwingine mitihani hiyo huwa migumu kiasi cha kumkatisha tamaa hata shujaa aliyevuka vikwazo vingi akiamini anakaribia kuishi kwa neema.

Uzoefu unaonesha kuwa watu wengi huporomoka na kupotea kabisa kwenye ramani ya safari ya mafanikio hasa baada ya kukutana na mitihani migumu na kuhisi huenda wamepangiwa kushindwa au wamerushiwa mikosi. Kila wanachokigusa kinashindikana, au kila wanapofanikiwa kidogo hutokea majanga na kuanguka tena.

Kutokana na hali hiyo, wengi hujikuta wakizalisha matatizo mengine makubwa zaidi baada ya kushindwa kuyadhibiti matokeo ya matatizo hayo. Hali hii hupelekea watu kupatwa na msongo mkubwa wa mawazo na hata wengine kuchukua hatua mbaya zaidi.

Lakini nini unachopaswa kufanya unapopatwa na ‘majanga’ mazito ili uweze kuinuka tena na kuanza safari? Nitakupa njia za jumla za kukabiliana na madhara makubwa ya tatizo ili tatizo hilo lisizue matatizo mengine kwa kushindwa kulitatua kwa njia sahihi.

  1. Tambua Chanzo 

Unachotakiwa kufanya kwanza unapopatwa na tatizo, tumia muda kadri inavyofaa kulifahamu vizuri tatizo lako na chanzo cha tatizo hilo ili ujue wapi pa kuanzia. Hii ni hatua ya kwanza kabisa na muhimu sana. Usipotumia muda wako kulitambua vizuri tatizo lako baada ya kupata taarifa, unaweza ‘kupaniki’ na kinachofuata ni uamuzi wa kukurupuka utakaozaa matatizo mengine mengi zaidi.

Kusanya taarifa zote muhimu kuhusu tatizo lako kwa umakini na utulivu ili ubaini kila unachotaka kukifahamu kuhusu tatizo hilo bila kuacha shaka.

Black businessman thinking at desk in office

Kufahamu vizuri na kwa umakini chanzo cha tatizo kitakusaidia wewe kuanza kufikiria njia bora zaidi ya kulitafutia utatuzi. Suluhisho la tatizo lolote lile huanza na utambuzi sahihi wa chanzo.

2. Kuwa na Fikra Chanya

Hatua ya pili, baada ya kutambua chanzo cha tatizo lako ni kujenga fikira chanya kuhusu tatizo hilo. Fikiria zaidi kuhusu uwezekano wa kulitatua zaidi ya kushindwa. Anza na fikira chanya

Kumbuka fikra hasi siku zote huwa chanzo cha kumtoa mtu mwenye matatizo kwenye ramani ya safari ya mafanikio na kujikuta akitumbukia kwenye tatizo jingine zito bila kutarajia. Baada ya hapo unapaswa kuwa na jibu la awali la hatua sahihi unayopaswa kuichukua.

3. Pima Kina cha tatizo

Ni muhimu sana kupima kina cha tatizo ulilonalo kwa mtazamo chanya. Kumbuka ulikotoka, ulipokuwa huna hata hicho ulichopoteza. Lifanye tatizo hilo la kutokuwa na kitu hata kidogo kuwa ndilo lilikuwa tatizo kubwa zaidi. Hivyo, kupoteza kile ulichokipata sio tatizo bali ni changamoto tu. Fikiria jinsi ulivyoweza kufika hapo wakati ukiwa huna uzoefu hata kidogo. Amini hivi sasa unaweza tena kurudi pale au kuvuka zaidi kwa kasi kwa kuwa una uzoefu wa kutosha na njenzo pamoja na maarifa.

Kumbuka mlango mmoja ukifungwa milango mingi zaidi hufunguka, lakini usipokuwa makini na kukurupuka utaona kiza tu mbele yako.

4. Washirikishe watu lakini ‘sio kila mtu’

Tatizo linapoonekana bado zito kwako, baada ya kutafakari tatizo lako na kuwa na mlengo chanya huku ukiwa na maswali kadhaa kichwani kuhusu tatizo hilo. Unapaswa kuwafikiria watu wako wa karibu ambao unawaamini na unahisi watakuwa washauri sahihi katika tatizo lililokupata. Wachague watu wawili kwa mfano ambao unawaamini. Wasikilize kwa makini na waambie ukweli ili ushauri wao ulenge ukweli uleule.

Kwa kuwa utakuwa umepitia hatua ya kulitambua vizuri tatizo lako na una majibu ya awali, ushauri wa watu hao unaowaamini utakusaidia kufanya maamuzi sahihi kwa mtindo wa ‘akili za mbayuwayu, changanya na zako.’ Hata hivyo, unashauriwa kuwa wakati unatafuta ushauri usidhani rafiki yako wa karibu ndiye mara zote atakuwa mtu sahihi zaidi wa ushauri. Kama tatizo lako ni la kitaalam, mtaalam wa eneo hilo atakuwa mtu sahihi zaidi.

Kwa nini uwaambie watu lakini sio kila mtu? Mchanganyiko wa mawazo ya watu wengi unaowaambia bila mpangilio yanaweza kukufanya uhisi unatatizo kubwa zaidi ya ulivyofikiria wewe. Wapo watu ambao huwa wana tabia ya kukatisha tamaa au kuonesha huruma iliyopitiliza hivyo kukufanya uhisi una tatizo zito sana. Hao ni watu wa kuwaepuka, kwa kuwa wataishia kufahamu tatizo lako na kukusikitikia tu hali itakayokuongezea majonzi zaidi.

Adviser

Ni muhimu kutambua kuwa hupaswi kabisa kukaa na tatizo moyoni mwako bila kushirikisha watu. Hali hii inaweza kukufanya uumie zaidi. Unapolisema tatizo lako unaufanya ubongo na moyo wako kupumua kwa kiwango cha juu sana na kuitoa sumu uliyoibeba.

5. Ikumbuke Imani yako

Imani yako ni kitu kikubwa sana unapokuwa kwenye matatizo. Muombe Mungu wako na jitahidi kutafuta vifungu vinavyozungumzia matatizo na jinsi Mungu alivyowasaidia waliokuwa kwenye matatizo hayo. Hii itakusaidia sana kuondoa msongo wa mawazo, kutulia na kutafuta njia sahihi ya kutatua tatizo lako. Muombe Mungu wako akupe ujasiri na utashi zaidi wa kukabiliana na changamoto hiyo na kukufungulia milango mingine. Amini hiyo inawezekana.

6. Chukua hatua, acha uoga

Baada ya hatua hizo ulizopitia, hakikisha kuwa unakuwa katika wakati mzuri wa kuchukua uamuzi kwa vitendo ili urudishe hali yako. Hatua hii ni muhimu sana kwa kuwa hatua zote za juu hazitakuwa na maana kama hautasimama tena na kuendelea kupambana na kuendelea na safari ya mafanikio, safari ambayo haina mwisho.

Hatari Yawakabiri Watumiaji Wa Simu Za ‘Iphone’
Tenga: Sitowania Tena Urais CECAFA