Mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang ataendelea kuwa chaguo la kwanza katika upigaji wa mikwaju wa peneti, kwenye kikosi cha Arsenal licha ya kutofanya hivyo wakati wa mchezo wa ligi dhidi ya Aston Villa, jana jumapili.
Arsenal walipata ushindi wa mabao matatu kwa mawili, na bao lao la kwanza lilifungwa kwa njia ya penati na mshambuliaji kutoka nchini Ivory Coast, Nicolas Pepe.
Meneja wa The Gunners Unai Emeri, amesema maamuzi ya nani alipaswa apige penati katika mchezo huo yalitolewa na Aubameyang, kwa kumkabidhi Pepe ambaye alifanikiwa kufunga bao la kusawazisha.
Amesema yeye kama meneja tayari ameshafanya maamuzi ya kumkabidhi jukumu Aubameyang, la kuhakikisha anapiga mikwaju yote ya penati inayotokea kwenye mchezo, na inapotokea jukumu hilo kapewa mtu mwingine hawezi kuingilia.
“Sijaona tatizo lolote kwa wachezjai wangu kukubaliana, Aubameyang ndio mwenye jukumu la kupiga penati, lakini kama aliridhia Pepe apige ni sawa.
“Nimeona hakuna kilichoharibika, na Pepe alipiga vizuri na tukafanikiwa kupata bao la kusawazisha.
“Kila mmoja kikosini anajua Aubameyang ndio chaguo la kwanza, na hakuna ambaye atalidharau hilo.” Alisema meneja huyo kutoka nchini Hispania.
Mbali na kukabidhi jukumu la mkwaju wa penati kwa Pepe, mshambuliaji Aubameyang alifunga bao la tatu na la ushindi dhidi ya Aston Villa, huku bao la pili likifungwa na Chambers.