Meneja wa klabu ya Arsenal Unai Emery amekanusha uvumi uliosambaa katika mitandao ya kijamii, kuhusu kusitisha mpango wa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Low wa kukutana na kiungo Mesut Ozil, kwenye eneo la uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo ya jijini London.

Emery amesema suala hilo halikutokea uwanjani hapo kama ilivyoelezwa jana katika mitandao ya kijamii, na anashangazwa ni nani alieanzisha uvumi huo, ambao amedai huenda uliandaliwa kwa lengo la kutaka kuvunja uhusiano uliopo kati yake na watu wa Ujerumani.

Taarifa zilizosambazwa jana zilieleza kuwa, meneja huyo kutoka nchini Hispania alikataa mpango wa kocha Low na meneja wa timu ya taifa ya Ujerumani Oliver Bierhoff, ambao wanadaiwa walifika kwenye uwanja wa mazoezi wa Arsenal kwa kusudio la kuzungumza na Ozil, ili kumbebeleza afute maamuzi ya kustaafu soka la kimataifa.

“Sio kweli kuhusu kinachoendelea katika mitandao ya kijamii, sikuzuia mpango huo,” alisema Emery alipohojiwa na Sky Sports.

“Sikuwa na tatizo na mtu yoyote katika mazoezi ya kikosi changu, na wala hakukua na jambo kama hilo. Sio kweli.”

Ozil alitangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya Ujerumani mwezi Julai, baada ya timu hiyo kuondolewa mapema kwenye fainali za kombe la dunia, na sababu kubwa alidai kuchoshwa na ubaguzi uliokua ukielezezwa kwake.

Kiungo huyo alisema mara kadhaa timu ya taifa ya Ujerumani ilipokua ikipoteza kwa kupata matokeo mabovu, alikua mmoja wa wachezaji wanaobaguliwa kwa asili yake ya Uturuki, huku picha aliyowahi kupiga na rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdoğan, ikitumika kama kielelezo.

JPM ataja sababu ya kuita Mfugale flyover
Taifa Stars itakayoikabili Cape Verde yatajwa