Kocha wa timu ya Arsenal Unai Emery amesema wana mpango wa kuwasajili wachezaji wenye thamani ya juu zaidi katika msimu ujao ili kukiboresha kikosi hiko
Kwa mujibu wa shirika la habari nchini Uingereza BBC, Emery amesema lengo lao ni kuwasajili wachezaji watatu au wanne ambao wataimarisha timu hiyo ambapo licha ya wachezaji wazuri waliopo ambao wanaweza kukisaidia kikosi chake lakini kuna hitaji la wachezaji wengine wenye thamani zaidi.
“Tunatafuta wachezaji wazuri sana na sasa tunazungumzia kuhusu uwezekano wa kuwasajili wachezaji maarufu na walio ghali,”alisema Emery.
Tayari maombi yao ya kutaka kumnunua winga wa Cryastal Palace Wilfried Zaha na beki wa kushoto wa Celtic Kieran Tierney yamekataliwa huku Arsenal tayari ikiwa imemsajili mchezaji raia wa Brazil Gabriel Martinelli lakini pia wanamuwinda beki wa Saint Etiene William Saliba japokuwa wapizani wao Tottenham Hotspur pia nao wanamuhitaji raia huyo wa Ufaransa mwenye miaka 18.
Hadi sasa wamewasilisha ofa ya £25m kumnunua mchezaji wa Scotland Tierney pamoja na £40m kumsajili mshambuliaji wa Ivory Coast na Crystal Palace Zaha ambaye amesalia na miaka 4 katika kandarasi yake na anadaiwa kuwa na thamani ya £80m.
Kocha wa Crystal Palace, Roy Hodgson amesema kwamba hadhani kama Arsenal wamewasilisha ombi ambalo limekaribia thamani ya kumnunua mchezaji huyo ambaye wanamuhitaji.
Bada ya kushindwa kufuzu katika mechi za mabingwa Ulaya, bajeti ya Arsenal imedaiwa kuwa £40m.