Meneja kutoka nchini Hispania Unai Emery amethibitisha kuondoka Parc des Princes mwishoni mwa msimu huu, baada ya kuitumikia PSG kwa miaka miwili.
Emery amethibitisha taarifa za kuondoka kwake akiwa katika mkutano na waandishi wa habari saa kadhaa zilizopita, ambapo amesema tayari ameshafanya mazungumzo na viongozi wa juu wa klabu ya PSG na wameafikiana kuhusu kuondoka kwake.
Emery alikichukua kikosi cha PSG mwaka 2016, baada ya kuisaidia Sevilla kutwaa ubingwa wa Europa League mara tatu mfululizo. Kuelekea kwake Parc des Princes kulikua na maana kubwa ya kuivusha PSG kwenye michuano ya kimataifa hususan katika suala la kutwaa ubingwa wa Ulaya.
“Nimeshazungumza na wachezaji kuhusu kuondoka kwangu,” amesema meneja huyo. “Ninamshukuru sana Rais wa klabu hii Nasser Al-Khelaïfi, Mkurugenzi wa michezo Antero Henrique, mashabiki na wachezaji wote niliofanya nao kazi kwa kipindi cha miaka miwili.
Mipango ya uongozi wa PSG chini ya meneja huyo imeshindwa kuzaa matunda kwa miaka miwili baada ya kikosi cha mabingwa hao wa Ufaransa kuondolewa katika hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu na Real Madrid, hali kadhalika msimu uliopita waliondoshwa na FC Barcelona.
Hata hivyo kwa upande wa ligi ya Ufaransa Emery ameweza kurejesha heshima ya klabu, kwa kutwaa ubingwa wa Ligue One msimu huu, ambao ulikua unashikiliwa na AS Monaco.