Picha ya hivi karibuni ya mtoto Divya iliyoibuka kuwa gumzo inayomuonyesha akiwa ameshikilia sufuria mkononi huku akisikiliza kwa makini kile ambacho watoto wenzake wanafundishwa darasani katika shule moja ya serikali imepelekea matokeo chanya.
Picha hiyo ambayo imegusa wengi ilichapishwa katika gazeti la ‘Telugu’ la tarehe 7 Novemba ikiwa na maandishi yanayosema “macho yenye njaa” iliibua hisia za watu kwa haraka,ambao waliona amekosa haki ya chakula na elimu, Kutokana na madai hayo, Divya aliandikishwa shule siku iliyofuata.
Imeelezwa kuwa Kuna utaratibu wa serikali wa kutoa chakula cha mchana katika shule zaidi ya milioni moja na watoto wadogo wanajua kwa sababu ndugu zao wanasoma huko ndiyo iliyomvuta mtoto huyo kwenda na sufuria.
Baba yake bwana Lakshman, kwa masikitiko makubwa amemwambia mwandishi wa BBC kuwa “Nilisikitika sana nilipoiona picha ya mwanangu gazetini, Divya ana wazazi ambao wanafanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maisha yake ya baadae lakini alionyeshwa kama mtoto yatima”
Divya na wazazi wake wanaishi kwenye chumba kimoja katikati ya mji wa Hyderabad, ambao wamesema kuwa walikuwa wanasubiri Divya kutimiza miaka sita ili wamuandikishe katika shule yenye hosteli ya serikali ambapo watoto wake wengine wawili wa kike wanaishi.
Pia wana mtoto mwingine wa kiume ambaye amemaliza sekondari na sasa ametuma maombi ya chuo huku akiwa anamsaidia baba yake kuokota taka.
Lakshman anajua changamoto anazopitia , yeye mwenyewe alikuwa bila wazazi na kila siku anapambana kupata maisha bora, Nyumba yao imezungukwa na makopo yaliyokatwa , tayari kwa ajili ya kuuza kufanyia uchakataji.
Anasema yeye na mke wake huwa wanapata kipato cha dola 139 kwa mwezi, fedha ambayo inanunua chakula chao na mavazi, Elimu ni bure kwa watoto kwa sababu shule ni za serikali.
Amesisitiza kuwa “Sikutaka watoto wangu wapitie maisha niliyoishi hivyo nilihakikisha kuwa wote wanaenda shule.” ambao ni pamoja na watoto wa kaka yake aliyefariki.
“Kaka yangu na mke wake walifariki hivyo ilinibidi nichukue jukumu la kuwalea kwa sababu sikutaka waishi kama watoto yatima, hivyo niliwaweka wote watano kwenye bweni na kuwatunza.”
Wanakijiji katika eneo hilo wanasema ukosefu wa shule ya awali hufanya wazazi kushindwa kupata sehemu ya kuwaacha ili waendelee na shughuli zao nyingine huku wakiwa na matumaini kuwa picha ya Divya itaweza kuchochea kuboresha mazingira ya shule, kwa kupatikana kwa mahitaji ya shule na lishe bora kwa watoto.
Hata hivyo Divya, amefurahia kuanza kwenda shule baada ya kupewa begi jipya la shule ambalo amekuwa akizunguka nalo kila mahali.