Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), limechangia kiasi cha shilingi 110 milioni katika kuwezesha huduma za maji kwa wananchi wa Jimbo la Kikwajuni kupitia Mradi wa Maji Kikwajuni uliozinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein miaka miwili iliyopita.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa UNDP, Alvaro Rodriguez wakati akizungumza na wananchi wa jimbo hilo baada ya kutembelea vituo na vyanzo vya mradi huo vya Migombani na Kilimani, amesema lengo lao ni kuona jamii zinapata huduma mbalimbali ili kuweza kuleta maendeleo na wao wanachangia kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni 110 ili mradi huo uweze kukamilika.
“Nimeridhishwa na maendeleo ya mradi unaotarajiwa kutoa huduma kwa wakazi zaidi ya 10,000 wa jimbo hili,UNDP inajitolea kiasi cha shilingi milioni 110 ili mradi huo uweze kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji,” alisema mwakilishi huyo wa UNDP
Naye Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Salama Abood Talib akizungumza kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, amesema lengo la serikali ni kuhakikisha inashirikisha wadau mbalimbali katika kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa wananchi wa maeneo mbalimbali visiwani humo na amemshukuru mwakilishi wa UNDP kwa msaada waliotoa katika kumalizia mradi huo.
Pia Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Mhandisi Hamad Masauni amesema mradi huo una awamu tatu huku awamu mbili zikiwa zishakamilika na wapo katika awamu ya mwisho ya kukamilisha mradi huo na amemshukuru mwakilishi huyo kwa msaada huo ambao utasaidia kukamilika haraka ili wananchi wafaidike na huduma hiyo.
Aidha, Mradi huo wa Maji Kikwajuni unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 344,000,000 ambapo awamu ya kwanza na ya pili ikiwezeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Mbunge wa Jimbo hilo, michango ya wananchi na Serikali ya Japan.
Mradi huo utakapokamilika utanufaisha wakazi zaidi ya 10,000 wa jimbo la Kikwajuni,visiwani Zanzibar.