Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, limelataka kufanyika kwa uchunguzi wa mauaji ya Mwandishi wa Habari, Ishtiaq Sodharo yaliyotokea eneo la Khairpur, Mkoa wa Sindh nchini Pakistan.
Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo Agosti 5, 2022 jijini Paris nchini Ufaransa, imesema Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay amelaani mauaji ya Ishtiaq Sodharo na kusema Waandishi wa habari wana jukumu muhimu la kuhabarisha jamii na haki yao ya kufanya hivyo lazima ilindwe.
Amesema, “Ninatoa wito kwa mamlaka kutumia juhudi zote kuchunguza sababu za mauaji ya Ishtiaq Sodharo na kuwafikisha Mahakamani wahusika wa mauaji yake ili watumikie adhabu inayostahili kwa mujibu wa sheria.”
Marehemu Sodharo, alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya kila wiki ya Sindhi Chinag, na inadaiwa kuwa alipigwa risasi nje ya nyumba yake Julai 1, 2022 na kufariki akiwa hospitali kutokana na majeraha aliyopata wakati wa shambulio hilo.
UNESCO inalaani mauaji hayo kwakua katika moja ya kazi zake ni kulenga kukuza usalama wa waandishi wa Habari, kupitia uhamasishaji wa kimataifa, kuwajengea uwezo na kwa kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wao.