Shirika la Kimataifa linalojihusisha na Idadi ya watu Duniani UNFPA, linatarajia kuzindua mpango wa kuwalinda vijana nchini Tanzania katika sekta muhimu zinazowahusu vijana ikiwemo suala la Maamuzi binafsi juu ya miili yao kuhusu Uzazi salama na Ushiriki wa mikakati ya kimaendeleo.
Katika mafunzo kwa waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam April 1, 2022, juu ya Mpango huo muhimu, Muwakilishi wa Nchi wa UNFPA, Mark Bryan Schreiner amesema Uswisi inathamini na kuzingatia uwingi wa vijana nchini Tanzania na hivyo kurasimisha mkakati wa kimaendeleo unaohusu vijana katika nyanza ya Afya, utawala na Uchumi.
“Hebu fikirieni ingekuwaje ikiwa vijana wote nchini Tanzania watakuwa na afya njema, wenye tija na kuwezeshwa. Hebu fikiria wakiwa huru kutokana na magonjwa yatokanayo na ngono, pamojanna Maambukizi mapya ya VVU, mimba zisizotarajiwa na ndoa za utotoni ikiwemo aina zote za ukatili. Fikiria wakiweza kupaza sauti zao na kutetea mabadiliko. Wafikirie vijana kama viongozi wa sasa wanaoweza kuendesha uvumbuzi na ukuaji wa uchumi. Huu ndio mustakabali ambao Uswisi na nathubutu kusema UNFPA na Serikali ya Tanzania wanaufikiria.” Mark
Afisa Vijana wa UNFPA, Fatina Kiluvia amesema mpango huu unalenga vijana ambao ni kundi kubwa walio katika balehe kwa kuwa wao ndio wanakumbwa na madhila mengi ya kidunia.
“Vijana balehe, zaidi ya milioni 57 nchini Tanzania ndio wanatarajia kunufaika zaidi kwa sababu wao ndio waathirika wakuu wa matatizo yanayohusu vijana, wao ndio wanakumbwa na ndoa za utotoni, wao ndio wanapata mimba za utotoni, wao ndio wanaacha shule kusaidia familia kiuchumi, wao ndio wanatoroka majumbani wakiona hawaelewi mazingira yale na huko waendako wanakutana na dunia katili zaidi,” amesema Fatina.
Mpango huu ambao utawahusu vijana kama kundi la kwanza, pia utawagusa wadau wote ambao wanahusika na vijana kama wazazi, viongozi wa dini, watunga sera, na viongozi wa mitaa na vijiji ambao ndio wakuu wa maeneo husika.
Fatina ameongeza kuwa lengo la mwishoni la mpango huu ni kuona vijana wanahusika katika utungaji wa Sera na mikakati yote ya nchi yanayohusu vijana, kuongeza uwezo na uchechemuzi wa kupanga sera rafiki kwa vijana, kuongeza ushiriki wa vijana katika kamati za maendeleo za maeneo yao, kuongeza uelewa wa elimu ya afya ya uzazi na kuongeza ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya vijana na dunia nzima katika kupeperusha bendera ya Taifa.
“Lengo Kubwa kabisa ni kuhakikisha kijana anaweza kuruka viunzi nyote vinavyokatisha ndoto zake, kijana aelewe fursa zilizopo eneo husika na aweze kushiriki kama ni mikopo, siasa za uchaguzi, Haki za kuamua juu ya uzazi salama, na kila namna awe amelindwa,” Fatina.
Kwa upande wake Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ubalozi wa Uswizi Tanzania, Leo Nascher, ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kukubali kujihusisha na UNFPA katika kuwashirikisha vijana kwenye maamuzi ya Sera na Afya ya Uzazi kwa upande wa Bara na Visiwani.
Mmoja wa vijana husika ambae amewakilisha vijana wengi, Gertrude Clement, Katibu wa baraza la Ushauri la vijana UNFPA amesema vijana wanashindwa kufanya maamuzi moja kwa moja kuhusu elimu ya afya ya uzazi kwa sababu jamii nyingi inaamini kijana mdogo hatakiwi kujihusisha wala kupata elimu hiyo hivyo Mpango huu utawasaidia kushiriki na kuwagusa vijana wengine wote kwa urahisi.
Mpango huu wa kuwalinda vijana utaanzia mikoa mitano ya Tanzania Bara na visiwani ambayo ni Kigoma, Shinyanga, Simiyu, Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar na Pemba.
Uzinduzi wa mpango huu wa kuwalinda vijana unatarajiwa kufanyika kwa usimamizi Ubalozi wa Uswizi Tanzania, Serikali ya Muungano wa Tanzania na shirika la Idadi ya watu Duniani UNFPA.