Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wakimbizi (UNHCR) nchini Uganda limesema kuwa lina wasiwasi mkubwa na fungu la fedha walilonalo kwa mwaka huu wa 2018.
Mwakilishi wa Shirika hilo nchini Uganda, Joel Boutroue amesema kuwa kufikia sasa wana asilimia 9% tu ya fedha wanazotaka katika bajeti yao ya dola milioni 450 walizopanga kutumia mwaka huu.
Amesema kuwa huenda shughuli za shirika hilo zikakwama kutokana na ukosefu wa fedha kutoka jamii ya kimataifa ambayo imekuwa ikitoa msaada mkubwa.
Aidha, Boutroue amesema kuwa kwa sasa wamepokea dola milioni 40 kutoka kwa wafadhili. na wanatarajia nyongeza ya fungu kutoka Geneva kwani wafadhili wanachagia mfuko wa UNHCR kuendeleza shughuli zao na baadaye inabidi warudishe fedha hizo.
“Kama hatutapata misaada zaidi tuko katika hali ya hatari, nikisema sisi ni wakimbizi na watu wote wanaohusika na katika suala hilo. Maana kama hatutapa fungu jingine mipango yote itaharibika. hatutaweza kuwalisha, kuwapa elimu na vingine bila ya vitu hivyo tunaweza kufikia katika hali mbaya zaidi,”amesema Boutroue
Hata hivyo, kila mkimbizi anayewasili nchini Uganda huwa anapewa kipande cha aridhi futi 50 kwa 50, vifaa vya ujenzi na mgao wa chakula, na pia wakimbizi wanaruhusiwa kufanya biashara kama ana uwezo wa kufanya biashara popote nchini akiwa na kitambulisho chake cha ukimbizi.