Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), limesema kutokana na ukata linashindwa kukidhi mahitaji ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na hivyo bila nyongeza ya ufadhili, litalazimika kukata mgao wa fedha na vifaa vya usaidizi kwenye kilimo, uvuvi na ufugaji.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa kitengo cha uhusiano wa nje UNHCR, Dominique Hyde hii leo Agosti 2, 2022 jijini Geneva Uswisi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia ziara yake nchini DRC na kushuhudia jinsi wakimbizi wanawake, wanaume na watoto wanahaha kuishi kwa machungu na vitisho na ukosefu wa fedha za usaidizi wa kibinadamu.
Amesema, wakati macho yote na masikio yameelekezwa kwenye majanga mengine makubwa kama Syria, Afghanistan na hivi sasa Ukraine, dharura nyingine, nyingi zikiwa Afrika zimeshindwa kuvutia usaidizi na rasilimali.
DRC, ni miongoni mwa operesheni za UNHCR ambazo hazijapatiwa ufadhili wa kutosha ambapo hadi tarehe 30 mwezi Juni mwaka huu wa 2022, ombi la ufadhili la mwaka hu ula dola milioni 225 limechangiwa kwa asilimia 19 pekee huku mahitaji yakiongezeka kila uchao.
Mwanzoni mwa mwaka huu, DRC ilikuwa inahifadhi wakimbizi na wasaka hifadhi zaidi ya 500,000 pamoja na wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 5.6 ambapo Hyde amesema mapigano kati ya jeshi la serikali, FARCD na vikundi vilivyojihami jimboni Kivu Kaskaizni vimefurusha watu wengine 160,000 kuanzia mwezi Aprili mwaka huu.
“UNHCR na wadau wake huko jimboni Ituri wamesajili zaidi ya vifo 800 kutokana na mashambulizi ya kutumia silaha na mapanga kwenye jamii huku mashambulizi hayo yakifurusha watu 20,700 kutoka makwao,” amefafanua Hyde.
Kutokana na ukata, asilimia 82 ya wakimbizi wa ndani hawatapokea msaada wa kutosha wa malazi hivyo watalazimika kuishi kwenye makanisa, shule na viwanja vya mpira au maeneo mengine ya wazi na wengine wanaweza kuamua kurejea nyumbani licha ya hatari ya kuweza kushambuliwa na makundi yaliyojihami.
Afisa huyo wa UNHCR amekumbusha kuwa, kila mtoto ana haki ya kupata elimu ya msingi, lakini kutokana na ukata huo ni asilimia 16 tu ya watoto ndio wana uwezo wa kwenda shule nchini DRC huku katika viwango vya sasa vya ufadhili, UNHCR ikishindwa kusaidia hata mtoto mmoja mkimbizi kwenda shule ya sekondari.