Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF limesema pamekuwa na ongezeko la mara tatu katika mashambulizi dhidi ya watoto kwenye maeneo yenye mizozo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Ripoti iliyotolewa leo na UNICEF imeeleza kuwepo zaidi ya visa 170,000 dhidi ya watoto, ambavyo ni sawa na visa 45 kwa siku katika maeneo yenye vita tangu mwaka 2010 katika kipindi cha miaka 10.
Miongoni mwa madhila wanayopitia watoto ni pamoja na mauaji, kukatwa viungo, kubakwa, kutekwa, kunyimwa huduma za kibinaadamu, kufanyishwa kazi na mashambulizi dhidi ya shule na hospitali.
Mwaka 2018 pekee, UNICEF iliorodhesha zaidi ya visa 24,000 vya uhalifu dhidi ya watoto, idadi ambayo ni mara tatu zaidi ya hali ilivyokuwa mwaka 2010.
Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore amesema watoto wanaotajwa kuwepo kwenye hatari zaidi ni kutoka Syria, Afghanistan na Yemen.