Biashara ya viroba imefikia ukingoni jijini Arusha baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Filex Ntibenda kupiga marufuku uuzwaji na unywaji wa kilevi hicho.

Ntibenda alitangaza kiama cha kinywaji hicho mkoani humo jana alipokuwa akizungumza na watendaji wa serikali za mitaa 145 za mkoa huo, maafisa watendaji wa kata 25 pamoja na wenyeviti wa serikali za mitaa.

Alisema kuwa unywaji wa viroba huchagiza watu kufanya kazi wakiwa wamelewa hususani madereva wa daladala, bodaboda na wapiga debe ambao hugeuka kuwa kero na kuongeza hatari katika kazi zao.

Alitahadharisha kuwa yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria mara moja.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa aliapa kulifanyia kazi sakata la mtuhumiwa mmoja wa dawa za kulevya mkoani humo anayedaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi na baadae kuachiwa katika mazingira yanayotatanisha.

“Huyu anayeuza dawa za kulevya halafu polisi wanamuachia na wananchi hawajui sababau za kumuachia halafu anaendelea kuuza dawa za kulevya… nasema mwisho wake umefika na nitamfuatilia kwa makini,” alisema.

Hivi karibuni, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma alisikika bungeni akitaka bangi ihararishwe huku akidai madhara ya matumizi ya viroba ni makubwa na hasi kuliko madhara ‘chanya’ ya matumizi ya bangi.

 

Mbowe aipongeza serikali ya Magufuli
TFF Kuwachukulia Hatua Kali,Viongozi Na Watumishi Wake