Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema anaamini Mbeya City itarejea kwa kishindo Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya timu hiyo kushuka kwa kupoteza mchezo wa ‘Play Off’ dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma.
Mbeya City inayomilikiwa na Halmashauri ya jiji la Mbeya, imeungana na klabu nyingine za jiji hilo Ken Gold na Mbeya Kwanza katika Mshike Mshike wa Championship msimu ujao 2023/24.
Homera amesema naamini Mbeya City na ina nafasi kubwa ya kurejea Ligi Kuu, kutokana na sifa ya mkoa wake kuwa bingwa wa kupandisha timu hivyo, wanaenda kujipanga upya kwa kurekebisha mapungufu ndani na nje ya uwanja kuhakikisha City inarejea tena.
“Kwanza mashabiki wawe na subra tunaenda kukaa kujadili namna ya kurejea upya, wachezaji walipambana ila haikuwezekana, tusilaumiane kwa chochote bali twende kusahihisha makosa,” amesema Homera.
Kwa upande wake Meya wa Halmashauri hiyo, Dourmohamed Issa alisema licha ya timu hiyo kukumbana na hujuma za hapa na pale lakini timu haipotei na badala yake wanaenda kuongeza nguvu ili kuirejesha tena.
“Tulidhulumiwa sana mechi nyingi hata hii ya Mashujaa (juzi) tunafunga mabao yanakataliwa, ila tumejifunza na tunaenda kujipanga kwa nguvu mpya kurudi tena, mashabiki wasikate tamaa,” amesema Issa.
Mmoja wa mashabiki wa soka jijini humo, Bartazari Juma amesema Mashujaa walijipanga mapema baada ya kuona nafasi ya kucheza ligi kuu ikiwa ni miaka mingi kushiriki ligi hiyo.
“Kuanzia ‘Play Off’ mkondo wa kwanza Mashujaa alikuwa anajipanga kwa yeyote, waliweka mipango.”