Uongozi wa Simba SC umeweka wazi kuwa, mpango kubwa ni kuandika rekodi nyingine ya kumvua ubingwa bingwa wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, Wydad AC ya Morocco.

Simba SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira maarufu Robertinho, leo Ijumaa (Aprili 28) ina kibarua cha kuhakikisha inatinga Nusu Fainali dhidi ya Wydad Casablanca ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo.

Katika Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali ya kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar, ubao ulisoma Simba 1-0 Wydad AC na mtupiaji alikuwa Jean Baleke.

Simba SC ina kazi ya kusaka ushindi ama kuulinda ushindi huo ili kutinga hatua ya Nusu Fainali kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa wanahitaji kuandika rekodi nyingine Afrika ya kumvua ubingwa bingwa mtetezi.

“Wengi wamesahau kwamba tuliwavua ubingwa Zamalek ile iliyokuwa kwenye ubora wake na baada ya hapo ikapotea kwenye ramani na sasa tunahitaji kuandika rekodi nyingine tena kwa kumvua ubingwa Wydad AC.”

“Ukweli upo wazi wapinzani wetu wametuzidi kwenye ubora na viwango lakini inapokuja suala la matokeo ya mchezo husika kinachoamua ni dakika 90 na sisi Simba tuna wachezaji wenye uzoefu wa kusaka ushindi, dua kwa mashabiki muhimu.”

“Tahadhari zote tunachukua licha ya kupata ushindi nyumbani, wengi wanalaumu tumepata ushindi mdogo ni kweli lakini inabidi ujue tumemfunga bingwa mtetezi sio kitu chepesi,” amesema Ally akiwa nchini Morocco

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2003, Simba SC iliivua ubingwa Zamalek katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, timu hizo zilipokutana hatua ya 16 bora.

Nyumbani jijini Dar es salaam Simba SC ilishinda 1-0, ugenini ikafungwa 1-0 lakini ikapenya kwa mikwaju ya Penati 3-2.

Serikali yahimiza utoaji taarifa matukio ukatili wa kijinsia
SIREFA: Singida tupo tayari kwa ASFC