Uongozi wa Simba SC umekiri kulipokea ombi la Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo Hassan Dalali la kutaka Wazee wa klabu kuzungumza na Wachezaji kuelekea mchezo wa Robo Finali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo Jumapili (April 17), Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya kucheza mchezo wa Mkondo wa pili Afrika Kusini Jumapili (April 24).
Mwenyekiti wa Simba SC upande wa Wanachama Murtanza Mangungu amesema Uongozi umesikia ombi la Mzee Dalali na unakwenda kulifanyia kazi kabla ya kulitolea maamuzi.
“Mzee wangu Dalali ombi lako tumelisikia, nitalifikisha kwa wenzangu tuangalie uwezekano wa Wazee kuongea na Wachezaji kabla ya mchezo wetu wa Jumapili.”
“Hata hivyo niseme wachezaji wameonyesha kujitambua kwa kucheza kwa nguvu na kuifikisha timu katika hatua ya Robo Fainali, tunapaswa kuwapongeza na kuendelea kuwapa hamasa ili waendelee kutupeleka mbali zaidi.”
“Ziada ya maneno kutoka kwa wazee tumeikubali, tutazungumza nao na kufanya utaratibu, lakini wanachama wote tunaomba muendelee kuwaombea wachezaji wetu waweze kutuwakilisha vizuri Uwanjani.” amesema Mangungu
Simba SC ilitinga Robo Fainali kwa kishindo kwa kuichapa USGN ya Niger mabao 4-0 kwenye mchezo wa Hatua ya Makundi, ikimaliza nafasi ya pili kwa kufikisha alama 10 sawa na RS Berkane ya Morocco.