Beki wa Pembeni wa zamani wa Simba SC Said Sued, ameutaka Uongozi wa Klabu hiyo kulitumia Dirisha Dogo la Usajili kufanya maboresho kwenye kikosi, kwa kusajili Mshambuliaji atakayesaidiana na Moses Phiri.
Simba SC inapitia wakati mgumu wa kuangusha alama inapocheza ugenini, ikifanya hivyo jana katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Mbeya City FC.
Said Swed amesema Simba SC inakosa Mshambuliaji makini ambaye ataweza kuisaidia timu inapocheza michezo migumu hasa ya ugenini, hivyo kuna ulazima kwa viongozi kufanya mpango wa haraka ili kumsajili mchezaji ambaye atafanya kazi moja na Moses Phiri.
Amesema alichokiona kwa sasa Mshambuliaji huyo wa Zambia anapewa majukumu mazito ya kufanya anapokua Uwanjani, lakini matokeo yake ni hafifu kufuatia anaocheza nao kutomuelewa ipasavyo.
“Simba SC atafutwe Mshambuliaji wa maana wa kucheza pacha na Phiri, kwani Phiri anapewa majukumu makubwa hadi wakati mwingine yanamchosha.”
“Wale waliopo hawaendani na kasi ya Phiri ndio maana hata akipangwa nao anapata shida wako taratibu.” amesema Said Swed
Tayari Uongozi wa Simba SC umeshathibitisha kuingia Sokoni wakati wa Dirisha Dogo la Usajili, ambalo litafunguliwa mwezi Desemba, ili kuboresha kikosi chao, ambacho kina deni kubwa la kurejesha heshima ya Ubingwa wa Tanzania Bara na kuvuka Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu 2022/23.