Uongozi wa Simba SC umesisitiza kutimiza mpango wa kuandika rekodi nyingine ya kumvua ubingwa bingwa wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, Wydad AC ya Morocco.
Simba SC inayonolewa na Kocha Mkuu kutoka nchini Brazil Roberto Oliveira ‘Robertinho’, kesho Ijumaa (Aprili 28) ina kibarua cha kusaka ushindi dhidi ya Wydad AC ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa wanahitaji kuandika rekodi nyingine Afrika ya kumvua ubingwa bingwa bingwa mtetezi.
“Wengi wamesahau kwamba tuliwavua ubingwa Zamalek ile iliyokuwa kwenye ubora wake na baada ya hapo ikapotea kwenye ramani na sasa tunahitaji kuandika rekodi nyingine tena kwa kumvua ubingwa Wydad.”
“Ukweli upo wazi wapinzani wetu wametuzidi kwenye ubora na viwango lakini inapokuja suala la matokeo ya mchezo husika kinachoamua ni dakika 90 na sisi Simba SC tuna wachezaji wenye uzoefu wa kusaka ushindi, dua kwa mashabiki muhimu.”
“Tahadhari zote tunachukua licha ya kupata, ushindi nyumbani, wengi wanalaumu tumepata ushindi mdogo ni kweli lakini inabidi ujue tumemfunga bingwa mtetezi sio kitu chepesi,” amesema Ally.
Ikumbukwe kuwa, mwaka 2003, Simba SC iliivua ubingwa Zamalek katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hizo zilipokutana hatua ya 16 bora.
Nyumbani Simba SC ilishinda 1-0, ugenini ikafungwa 1-0, lakini ikapenya kwa penalti 3-2.
Katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Simba SC ilichomoza na ushindi wa 1-0, likifungwa na Jean Baleke.
Kesho Ijumaa (Aprili 28) Simba SC ina kazi ya kusaka ushindi ama kuulinda ushindi huo ili kutinga hatua ya Nusu Fainali kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo.