Uongozi wa klabu ya Tabora United umeshangazwa na beki Mghana, Asante Kwasi aliyeamua kupeleka kesi yake Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ na klabu hiyo kufungiwa kufanya usajili.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora, Thabiti Kandoro amesema kuwa wameshangazwa na hilo sababu walikuwa wakimlipa mchezaji wao huyo wa zamani kidogo kidogo kwa makubaliano lakini ghafla ameamua kwenda FIFA.

Hiyo ni baada ya juzi Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, kueleza kuwa klabu hiyo imefungiwa na FIFA kufanya usajili mpaka itakapomlipa Kwasi madai yake ya ada ya usajili na malimbikizo ya mishahara.

“Kilichotokea ni hali ya kawaida lakini tumeshangazwa kwa nini amefika (Kwasi) huko wakati tulikuwa na makubaliano na tulishamlipa kiasi kikubwa bado kidogo tumalizane, kiasi kilichobaki ni kidogo na tutamaliza hilo deni baada ya mechi yetu na Coastal Union (iliyochezwa jana),” amesema Kandoro.

Amesema kwa sasa timu hiyo ipo kwenye makubaliano na wachezaji wake kadhaa wa awali ikiwa katika kumaliza madeni mbalimbali ya timu hiyo kama ilivyomalizana na aliyekuwa kocha wao, Ahmed Soliman raia wa Misri takribani miezi miwili iliyopita.

Manuel Neuer amerejea Bayern Munich
FC Barcelona yatangaza faida 2022/23