Uongozi wa klabu ya Simba na benchi la ufundi, kwa pamoja unawashukuru sana wanachama, washabiki wake na watu wote waliohudhuria kwenye sherehe za miaka 80 ya klabu yetu ambazo zilijumuisha kilele cha wiki ya Simba Day ambazo zilifanyika Jumatatu tarehe 8-8-2016 katika uwanja wa Taifa.

Pia uongozi wa Simba unawashukuru sana kwa ushangiliaji wenu wa ‘NGUVU’ uliochagiza ushindi mnono wa magoli 4-0 dhidi ya timu kongwe kutoka Kenya AFC Leopards.

Washabiki wetu mmeonesha tofauti kubwa baina yao na sisi, kuujaza uwanja kiasi kile kwa viingilio vyenu wenyewe na sio kuingizwa ‘BURE’ ilhali timu imetoka katika msimu ambao haukuwa na matokeo ya kuridhisha sana ni ishara kuwa mna mapenzi makubwa sana na klabu yenu na uongozi unaamini hilo ni deni kubwa linalopaswa kulipwa kwa kuwapa furaha katika msimu huu wa ligi 2016/17.

Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha wale wanaotubeza, eti Leopards inashika nafasi za chini kwenye ligi kuu ya Kenya na ndio maana tukawafunga 4-0. Wajiulize wao Medeama waliowapiga ‘thalatha’ wanashika nafasi ya ngapi kwenye ligi yao wakati wanawapa kile kisago cha mbwa mwizi?

Kimsingi timu mwalikwa kwenye tamasha la Simba Day lazima iwe inacheza ligi kuu ya kwao na iwe timu yenye historia iliyotukuka katika soka…AFC Leopards ni timu iliopo katika ligi kuu nchini Kenya na historia yake kwenye soka la Afrika huwezi kuilinganisha hata kidogo na Medeama ambayo iliwadhalilisha ‘WAKODISHWAJI’.

Mwisho niwafahamishe kuwa timu yenu itaendelea na mazoezi kesho Jumatano pale Police Kilwa road na weekend hii itaingia kambini tayari kwa mchezo wa kwanza wa ligi kuu inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

 

Imetolewa na

Haji S. Manara

Mkuu Wa Habari

Simba Sports Club.

Simba Nguvu Moja

Naibu Waziri Mpina Aiasa Taasisi Ya Muungano Kufanya Tafiti Zenye Tija Kwa Serikali Na Umma
Frank de Boer: Nitarejeshea Heshima Inter Milan