Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi amesusiwa kazi ya kufanya maamuzi nani anapaswa kukatwa katika kipindi hiki cha Usajili wa Dirisha Dogo, ili kupisha maingizo ya Wachezaji wawili wa Kimataifa wanaopigiwa chepuo kusajiliwa Klabuni hapo.
Young Africans kupitia kwa Rais wake Injia Hersi Said tayari imeshathibitisha itasajili wachezaji wawili wa Kimataifa ambao watakiongezea nguvu kikosi chao, katika harakati za kuwania ubingwa na kushiriki ipasavyo kwenye Mshike Mshike wa Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Usajili wa wawili hao unapaswa kufanywa ndani ya kipindi hiki, huku kukiwa na wachezaji 12 wa kigeni waliosajiliwa Klabuni hapo, hivyo wanapaswa kupunguzwa.
Wachezaji wa Kigeni wa Young Africans waliopo kikosini hadi sasa ni Djigui Diarra, Joyce Lomalisa, Djuma Shaban, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Jesus Moloko, Bernard Morrison, Stephane Aziz Ki, Heritier Makambo, Fiston Mayele, Gael Bigirimana na Tuisila Kisinda.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa Wachezjai wengine wawili wa Kigeni ambao hawakuwa sehemu ya waliosajiliwa kwa mujibu wa Kanuni za TFF Lazarous Kambole na Yacouba Songne wamepona baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha yaliyokuwa yakiwakabili, hivyo wanafanya idadi ya wachezaji wa Kigeni kuwa 14.
Rais wa Yanga, Hersi Said, amesema Kambole na Yacouba walikuwa majeruhi na wamepona na kuhusu nani abaki hilo ni jukumu la kocha kulingana na mahitaji ya kikosi chake kuelekea katika Michuano iliyoko mbele yao.
Amesema kulingana na idadi ya wachezaji 12 wa kigeni wanaotakiwa kusajili kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka nchini (TFF), wanalazimika mmoja kuondoka kwa sababu wataongeza nyota wawili wengine wawili wa kigeni katika Dirisha hili Dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 16, mwaka huu.
“Kulingana na idadi ya wachezaji wa Kigeni, tunalazimika mmoja kuondolewa hilo tumemuachia Nabi, kati ya Yacouba na Kambole nani atabaki, pia tumepokea maombi ya mikopo kwa baadhi ya wachezaji wetu kutoka klabu zingine na tutawaruhusu kwenye Dirisha hili Dogo.
“Huu ni wakati wetu Young Africans kuweka alama kwenye mashindano ya kimataifa, mfumo wetu ni uleule mchezaji tunayemsajili lazima awe bora sana au zaidi ya yule ambaye tunaye,” amesema Hersi.