Uongozi wa klabu ya Young Africans umetoa shukurani kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kwa kuonyesha ushirikiano wakati wote wa Mapambano ya Mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Young Africans ilimaliza michezo ya mzunguuko wa kwanza Jumatano (Februari 23) kwa kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-0, na kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 39.
Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya klabu hiyo Kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Hassan Bumbuli ametoa shukurani hizo kwa niaba ya Uongozi mapema leo Jumamosi (Februari 26), alipohojiwa na Azam TV.
Bumbuli amesema wanaamini mafanikio waliyoyapata hadi kumalizika kwa Mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara yametokana na ushirikiano mkubwa ulioneshwa na Mashabiki na Wanachama wao, ambao siku zote wamekua wakiiombea mema timu yao.
“Haikua ujanja wetu kufikia mafanikio haya kwa kucheza michezo ya Mzunguu wa kwanza bila kupoteza, tunaamini Mashabiki na Wanachama wamechangia kwa kiasi kikubwa, hatuna budi kuwashukuru katika hilo.”
“Bado tuna kazi kubwa katika Mzunguuko wa pili ambao tutauanza kesho Jumapili (Februari 27) kwa mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar, tunahitaji nguvu kutoka kwa Mashabiki na Wanachama wetu kama ilivyo kawaida yao. Tunaamini tukiendelea kwa mshikamano huu tutafikia lengo la kuwa mabingwa msimu huu.” Amesema Bumbuli
Young Africans imeusotea Ubingwa wa Tanzania Bara kwa misimu minne mfululizo huku wakishuhudia watani zao Simba SC wakinyakua ubingwa huo katika kipindi chote na kushiriki Michuano ya Kimataifa kwa mafanikio makubwa.