Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema suala la kupanda miti ni lazima na kuzitaka Halmashauri zote nchini kusimamia kwa karibu na kuhakikisha kwamba mazingira ya maeneo yao yanakuwa ya kijani, safi na ya kuvutia na zoezi hilo liwe endelevu.
Dkt. Mpango, ameyasema hayo hii leo Machi 27, 2023 wakati wa akizundua kampeni ya kupanda miti kitaifa ikishirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), uliofanyika katika eneo la Mtumba Jijini Dodoma.
Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wanapaswa kutoa maelekezo kwa shule, taasisi mbalimbali na kwa wananchi ili washiriki kikamilifu katika uhifadhi na usafi wa mazingira.
Aidha, Makamu wa Rais pia ameziagiza Halmashauri kwa kushirikiana na TFS, kupanda aina za miti ambayo inaendana na mazingira ya maeneo waliopo pamoja na kuiwezesha jamii hususani ya vijana kupata elimu zaidi kuhusu utunzaji wa miti ili kuhakikisha wanachangia katika uhifadhi wa mazingira kwa weledi.
Hata hivyo, Dkt. Mpango pia ametoa wito kwa taasisi hizo kuongeza juhudi hasa katika kuhamasisha, kukuza uelewa na kujenga uwezo wa jamii na taasisi mbalimbali kuhusu hifadhi ya mazingira pamoja na kutafuta rasilimali fedha zitakazo changia utekelezaji wa Sera ya Mazingira.
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amesema ajenda ya upandaji ya miti inalenga kupanda miti milioni 1.5 kwa kila Halmashauri na miti milioni 40 kwa mkoa wa Dodoma pekee katika kipindi cha miaka mitano.