Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (TAOMAC) wamekutana na Waziri wa Nishati, January Makamba katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, ikiwa ni jitihada za kuendelea kuhakikisha bidhaa ya mafuta ya Petroli inapatikana kwa uhakika maeneo yote nchini.
Katika kikao hicho cha Agosti 4, 2023 TAOMAC walitoa taarifa ya mwenendo wa biashara ya mafuta duniani na hapa nchini pamoja na kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mafuta hususani suala la upatikanaji wa dola za Marekani.
Aidha, TAOMAC pia ilifafanua kuwa uhaba wa dola za marekani katika soko la fedha kunapelekea waagizaji kupunguza kiasi cha mafuta wanachoagiza kuepuka kuagiza mzigo na kushindwa kuulipia kwa wakati jambo ambalo linaongeza gharama za uendeshaji wa biashara na kuathiri bei ya mafuta kwa mteja wa mwisho.
Makamu Mwenyekiti wa TAOMAC, Salim Baabde alisema, “biashara yetu inafanyika kwa kutumia Dola za Marekani na inapotokea dola inakuwa adimu sokoni inaathiri moja kwa moja bei ya uagizaji ambayo mwisho wa siku inaathiri bei ya mafuta kwa mtumiaji wa mwisho.”
Aidha, alisema hali inaweza kuzidi kuwa mbaya iwapo changamoto ya upatikanaji wa dola haitatuliwa kwa haraka huku wakiiomba Serikali kuongeza nguvu katika kuhakikisha dola zinapatikana kwa kushirikisha benki za biashara ili kuepuka changamoto hii kukuwa zaidi na kuleta athari kubwa” aliongeza Ndugu Baabde.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAOMAC, Raphael Mgaya alimhakikishia Waziri Makamba kuwa pamoja na changamoto hiyo, wataendelea kuagiza mafuta ingawa kwa gharama kubwa ili kuhakikisha nchi inaendelea kupata nishati hiyo muhimu katika hali ya uhakika na endelevu.
Amemshukuru Waziri na EWURA kwa ushirikiano wanaoutoa kwa tasnia hasa katika vipindi vigumu na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali pamoja na kuelimisha umma kuhusu biashara ya mafuta ili kukabiliana na upotoshaji mkubwa hasa mitandaoni kuhusu biashara hii.
Kwa upande wake Waziri Makamba amewashukuru kwa ushirikiano waliutoa kuhakikisha nchi inapata mafuta muda wote na kusema mlango wake uko wazi wakati wote kwa ajili ya mashauriano.
Aidha, Waziri Makamba alisisitiza kuwa Serikali inaelewa changamoto ambazo sekta inakabiliana nazo kwa sasa na kuwa hatua madhubuti zimeendelea kuchukuliwa. Aidha Mhe. Makamba alisisitiza umuhimu wa wadau ikiwemo TAOMAC kuendelea kushikamana na kushirikiana ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta kwa uhakika kwa ajili ya ustawi wa nchi na watu wake.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Petroli na Mafuta Ndg. Michael Mjinja, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dr. James Andilile na wataalamu kutoka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).