Licha ya uwepo wa changamoto za hali ya hewa, hali ya upatikanaji wa chakula cha kutosha katika maeneo yote nchini imeendelea kuimarika ambapo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023, uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa ulikuwa tani milioni 17.4 ikilinganishwa na mahitaji halisi ya tani milioni 15.1.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma hivi karibuni, na kuongeza kuwa, uzalishaji huo umeihakikishia nchi utoshelevu wa chakula kwa asilimia 115 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024.
Amesema, “pamoja na uwepo wa ziada ya mazao ya chakula nitoe wito kwa Watanzania kuhifadhi mazao ya nafaka kwani utengamano wa hali ya chakula nchini umeendelea kuwepo kutokana na ziada inayotokana na mazao yasiyo ya nafaka.
Waziri Mkuu amesema, Serikali pia imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha hali ya chakula inaendelea kuimarika ambapo hadi kufikia Januari, 2023, tani 29,084.21 za mahindi zilisambazwa katika Halmashauri 59 zilizopata changamoto ya upungufu wa chakula kwa mwaka 2022/2023. Mahindi hayo yaliuzwa kwa bei ya chini ya soko ili kuimarisha upatikanaji wa chakula katika maeneo hayo.
Aidha, sambamba na hatua hizo, Serikali imeendelea kuratibu upatikanaji wa mbolea, mbegu bora na viuatilifu kwa wakati ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo. Hadi Februari, 2023 upatikanaji wa mbolea umefikia tani 407,333 sawa na asilimia 58.33 ya mahitaji ya tani 698,260.