Hatimaye mchakato wa kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM kuwania kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu, Oktoba mwaka huu, umehitimishwa katika ukumbi wa Convention Centre ambapo John Pombe Magufuli ametangazwa rasmi kuipeperusha bendera ya chama hicho.

Akitangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huo kwa ridhaa ya mwenyekiti wa CCM, spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda alisema zoezi la kuhesabu kura lilikamilika vizuri ambapo jumla ya kura 2422 zilihesabiwa.

“Kura zilizopigwa zilikuwa 2422. Kura zilizoharibika zilikuwa 6, kwa hiyo zikabaki kura halali 2416. Baada ya kuchambua na mawakala wetu (anawataja), Dr. Asha Rose Migiro alipata kura 59, hii ni sawasawa na asilimia 2.4. Mheshimiwa Balozi Amina Ali alipata kura 253, sawa na asililimia 10.5,” alisema Spika Makinda.

“Nilonge nisilonge!!” Alisikika Makinda huku akivuta pumzi kwa furaha. “Mh. John Pombe Magufuli alipata kura 2104, sawa na asilimia 87.1. Kwa hiyo, mheshimiwa John Pombe Magufuli ndiye aliyeibuka kidedea katika uchaguzi huu,” alimaliza.

Matokeo hayo yalizua shangwe kubwa ukumbini hapo na watu walianza ‘kuserebuka’ na nyimbo za kundi la ToT. Mchakato wa kumpata mgombea mwenza ulianzishwa haraka ambapo viongozi wa ngazi za juu wameingi katika kikao kingine kushauriana jina litakalomsindikiza Magufuli kwenye mbio za urais katika uchaguzi mkuu, Oktoba mwaka huu.

Tanzia: Mzee Ojwang Wa Vitimbi Afariki
Dodoma: Magufuli Ashinda Kwa Kishindo Kugombea Urais CCM