Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikise amesema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na huenda kukawa na maendeleo ya kuisikiliza kesi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ikitarajiwa kutajwa leo octoba 25, 2022.
Wikise amesema Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Sabaya ambapo mwanzo kulikuwa na wastakiwa watano wengine walikiri kosa na akabaki sabaya huwezi endelea na kesi kama ilivyokuwa.
“Upelelezi umekamilika, unajua shida ni kwamba mwanzoni walikuwa washtakiwa watano lakini wengine walikiri makosa na akabaki Sabaya, sasa huwezi kuendelea na kesi kama ilivyokuwa mwanzo, ni lazima tufanye adjustments (marekebisho),” amesema Wikise
“Mimi naamini wiki ijayo (leo) kutakuwa na progress (maendeleo), upelelezi ulikuwa umekamilika wakati ule wale walipokiri makosa, lakini yeye Sabaya hakukiri sasa tulitakiwa kufanya marekebisho,” amesema Wikise
Kuahirishwa kwa shauri hilo mara kwa mara kumewafanya mawakili wa Sabaya kuhoji kwa nini kila wakati inapotajwa na upande wa mashitaka kuieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika, wakati siku ya kwanza walisema umekamilika.
Oktoba 10, wakili wa utetezi, Hellen Mahuna aliibua hoja hiyo na kuutaka upande wa mashtaka kufuata mwongozo uliotolewa na DPP kukamilisha upelelezi ndani ya siku 90.
Wakili upande wa mashitaka, Suzy Kimaro aliieleza mahakama kuwa mwongozo uliotolewa na DPP umeanza kutumika Oktoba mosi mwaka huu hivyo hawako nje ya muda tangu utolewe.
Hata hiyvyo, Wakili Hellen amesema kama kuna jambo upande wa mashitaka wanatakiwa kulifanya kutokana na mwongozo huo walifanye na wasitegemee una siku 10 tu, waangalie shauri lilifikishwa lini mahakamani hapo mara ya kwanza.
Kesi hiyo inayopelelezwa na Takukuru, waendesha mashitaka wake wanashirikiana na wale wa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.
Sabaya atakuwa ametimiza siku 145 akiwa gerezani tangu afikishwe mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni mosi akiwa na washitakiwa wenzake wanne ambao waliachiwa baada ya kukiri makosa waliyoyatenda na kulipa faini.