Wafanyakazi wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited – GGML, wamejitokeza katika maonesho ya sita ya teknolojia ya madini Geita na kupatiwa elimu pamoja na uchunguzi wa ugonjwa wa Saratani.

Akizungumzia utoaji wa huduma hizo, Mratibu wa huduma za Tiba katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Geita, Dkt. Pasclates Ijumba amesema lengo ni kudhibiti madhara ya saratani hususani kwa wananchi ambao wamekuwa waoga kufanyiwa uchunguzi kutokana na na dhana potofu iliyojengeka ndani ya jamii.

Mratibu wa Idara ya Huduma za dharura kutoka GGML, Evarist Mwanakatwe akipatiwa vipimo vya saratani ya tezi dume kutoka kwa mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita.

Amesema “chanjo ya Saratani ya shingo ya kizazi imekuwa ikitolewa kwa mabinti wadogo, lakini baadhi ya jamii huwazuia watoto wao kupatiwa chanjo hiyo kutokana na ukosefu sahihi wa elimu kuhusu chanjo hiyo, pia niwatoe hofu wanaume kwamba sasa kuna kipimo maalumu cha damu badala ya kipimo cha kidole na tayari baadhi ya wafayakazi hao wa GGML wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya tezi dume.”

Mmoja wa wafanyakazi hao Evarist Mwanakatwe amesema wamehamasika kufanyiwa uchunguzi wa saratani na kupatiwa elimu, huku Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML, Dkt. Kiva Mvungi akisema saratani ya tezi dume inashika nafasi ya pili kwa aina ya saratani zinazowapata wanaume na inashika nafasi ya sita kwa kusababisha vifo vitokanavyo na saratani Duniani.

Mmoja wa wanyakazi wa Idara ya Huduma za dharura kutoka GGML, Sande Misenya akipatiwa vipimo vya saratani ya tezi dume kutoka kwa mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita.

Amezitaja dalili kuu za saratani ya tezi dume kwa wanaume ni kushindwa kupata haja ndogo, kukojoa damu wakati mwingine wanapata maumivu ya mgongo na nyonga na kudai kuwa idara ya afya, usalama na mazingira pamoja na idara ya mahusiano ya jamii kutoka GGML imeandaa kampeni ya kupima saratani na kuimarisha uelewa.

Mtaalam wa maabara kutoka Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita, Deogratias Keeka (kulia) akimpatia huduma za vipimo vya saratani, Dereva kutoka GGML, Andrew Elias.

Kampeni hiyo, imelenga kutoa elimu na kupima saratani kwa wafanyakazi wa GGML na jamii inayozunguka mgodi huo ili kila mtu apime afya yake na iwapo akigundulika kuwa na tatizo hilo aweze kutibiwa mapema ambapo katika maonesho hayo, kwa mwaka huu yamejumuisha zaidi ya washiriki 400, yatafanyika kwa muda wa siku 10 kuanzia tarehe 20 hadi 30 Septemba mwaka huu.

Huduma ya elimu na uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, matiti na tezi dume inatolewa bure na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya GGML katika viwanja vya Bombambili vilivyopo kwenye eneo maalumu la ukanda wa uwekezaji (EPZA) mjini Geita.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 25, 2023
REA yafanikisha utekelezaji mradi wa Umeme Kilolo