Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga amefanya ziara katika Kituo kidogo cha Kuzalisha Umeme kwa Gesi Asilia kilichopo Tegeta Jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 2, 2023.
Akizungumza baada ya kukamilisha ziara hiyo Naibu Waziri amesema Kituo hicho chenye mitambo mitano inayozalisha Megawati 43 ambapo ni Megawati 8.5 kwa kila mtambo ma kusema mtambo mmoja kati ya mitano upo nje ya kituo kwa ajili ya matengenezo ya lazima ambapo unatarajiwa kurejeshwa hivi karibuni.
Amesema “hali ya uzalishaji inaendelea vizuri, nimewaelekeza TANESCO kuhakikisha matengenezo ya mitambo ya lazima yanafanyika kwa wakati na ndani ya muda mfupi pamoja na ukaguzi huo, nimewaelekeza kuimarisha huduma kwa wateja, wahakikishe wanatatua changamoto kwa wakati, yaani watoe huduma balimbali kwa wakati pindi kunapotokea hitilafu, wale wenye uhitaji wa kuunganishiwa umeme nao wapewe huduma.
Kuhusu changamoto ya gesi amesema zipo kadhaa na wanapambana nazo, lakini akagusia kuwa uzalishaji wa umeme kwa njia ya maji licha ya kuwa na changamoto kadhaa lakini ni wa bei rahisi ndio maana ni sehemu ya mipango ya kuzalisha umeme.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga akizungumza wakati wa ziara hiyo kwenye Kituo kidogo cha Kuzalisha Umeme kwa Gesi Asilia.
Amesema “Kwa sasa Shirika la Umeme la Tanzania (TANESCO) linashirikiana na Wizara ya Nishati tunafanyajitihada kuwa na umeme wa uhakika kwa ajili ya Wananchi kawaida na kwa ajili ya shughuli za uzalishaji pia umeme upatikane kwa gharama nafuu.
“Wiki iliyopita tulisema kwenye Gridi ya Taifa kuna upungufu wa Megawati 400, hizi huwa zinacheza kulingana na mahitaji ya siku husika, juhudi zinaendelea na kupata gesi zaidi kutoka kwenye visima vyetu wakati huohuo kuna matengenezo ya mitambo na ripoti ya kufikia leo upungufu kwenye Gridi ni Megawati 300 hadi 350, pamoja na hivyo kusudio letu ni kuwa hadi kufikia Machi 2024 tusiwe na changamoto ya upungufu.”