Ikiwa imesalia miaka mitatu kufikia Uchaguzi Mkuu wa 2025, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Masoud Othman Masoud ameeleza kuwa anakutana na maswali ya sintofahmu kutoka kwa wananchi na wanachama wa ACT-Wazalendo.
Akizungumza hivi karibuni kwenye mahojiano maalum na Dar24 Media ofisini kwake visiwani humo, Makamu wa Kwanza wa Rais alisema kuna hali ya sintofahamu, kwakuwa baadhi ya watu hawafahamu kitakachotokea visiwani humo baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
“Bado kilichopo ambacho kinaonekana wazi kwa watu ni kutokua na uhakika wa nini kinakuja na hali itakuaje 2025. Hayo ni maswali ya watu unayapata kila siku na hata yasiposemwa unasikia sauti zake kwa sababu unayaona mashaka mashaka,” Othman ameiambia Dar24 Media.
Akizungumzia uwepo wake kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema kuwa ana uhusiano mzuri na Rais Mwinyi kwa ajili ya maslahi ya wananchi, lengo kuu likiwa kuenzi hali ya amani waliyoachiwa na Hayati Maalim Seif.
“Rais mwenyewe ana pande mbili, ana Serikali na ana siasa,” Othman ameiambia Dar24.
“Kwa wale waliopo Zanzibar wanafahamu kwa urahisi, kuna mambo anayoweza kuyafanya na kuna asiyoweza kuyafanya. Kwahiyo, tunaishia pale ambapo ‘limitations’ zilizopo tunazifanyia kazi,” ameongeza.
Machi 1, 2021 Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar baada ya kushauriana na chama cha ACT -Wazalendo, alimteuwa Othman Masoud kuwa makamu wake wa kwanza kuchukuwa nafasi ya Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.
Angalia mahoajiano kamili na Dar24 Media hapa: