Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo – CENI, imetangaza kuwa wagombea 24 akiwemo Rais wa Taifa hilo Felix Tshisekedi, watagombea urais wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Desemba 2023.
Wapinzani wa zamani, Wagombea wa mara ya kwanza na Wagombea walioshindwa katika chaguzi zilizopita ni miongoni mwa wanaopinga utawala wa Rais Tshisekedi na kufanya uwepo wa idadi kubwa ya wagombea ambayo huenda ikagawanya kura za upinzani na kuimarisha nafasi ya ushindi kwa Tshisekedi.
CENI, ilichapisha wasifu wa wagombea hao 24 katika mtandao wake wa kijamii wa X, ambao awali ulijulikana kama Twitter na sasa Mahakama ya kikatiba itathibitisha rasmi orodha ya mwisho katika wiki chache zijazo.
Hata hivyo, Mchambuzi wa masuala ya Kisiasa wa kituo cha utafiti cha Ebuteliu, Tresor Kibangula amesema mazungumzo yanaendelea miongoni mwa baadhi ya wagombea ili kuungana na kumuunga mkono mpinzani mmoja maarufu.