Urejeshaji wa miundombinu ya barabara iliyokuwa imeharibiwa na maporomoko ya matope na mawe yaliyotokea Desemba 3, 2023 katika Mji wa Katesh uliopo Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara umefikia asilimia 75.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Godfrey Kasekenya Mkoani Manyara, mara baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa kazi hizo zinazofanywa na Wakala ya Barabara (TANROADS) wakishirikiana na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
“Hadi sasa tumefikia karibu asilimia 75 ya kuirejesha Katesh katika hali yake na tutakachofanya kabla ya kuondoka tutakuwa tumehakikisha tumesafisha barabara zote na kuzirudisha katika hali yake ya awali kama tulivyokuwa tumeagizwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Kasekenya.
Kasekenya ameongeza kuwa mitambo na magari imeshafika eneo la Katesh ambapo kuna magari 32 yenye uzito wa tani 13, vijiko 12, doza 3, magari ya kishindilia barabara miwili, mitambo ya kubeba matope (roller) miwili, na mitambo yote hiyo inaendelea kufanya kazi usiku na mchana.
Amesema Wizara hiyo kupitia Wakala hizo wanaendelea kufungua barabara za mitaa kwa ajili ya kuhakikisha njia zinafunguka kwa kutoa mawe na magogo ili kuhakikisha kama kuna mali za watu zilisalia katika makazi yao wanaweza kuingia na kufanya usafi.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema kuwa mbali na Serikali kurejesha miundombinu pia imeendelea kuwa bega kwa bega na Wananchi.