Tunaanza kuzimulika timu za kundi D zilizofuzu kuingia kwenye kinyanyanyiro cha fainali za Kombe la Dunia mwaka huu nchini Urusi. Kundi hili lina timu za Argentina, Iceland, Croatia na Nigeria. Na leo tunaanza na Argentina.

Argentina imefuzu fainali za kombe la dunia ikitokea ukanda wa Amerika ya Kusini wenye mataifa ya Colombia, Chile, Paraguay, Peru, Brazil, Ecuador, Venezuela, Bolivia, Peru na Uruguay.

Argentina ilimaliza kundi la ukanda huo kwa kufikisha alama 28 ambazo ziliwaweka kwenye nafasi ya tatu, nyuma ya Uruguay waliokuwa na alama 31 na vinara Brazil waliofikisha alama 41.

Katika michezo 18 ya kundi hilo, Argentina ilishinda michezo 7, kutoa sare michezo 6 na walipoteza michezo mitano.

Kanuni za ukanda wa Amerika ya Kusini kuwasilishwa na timu tano, ziliibeba Argentina hadi kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018.

Majina ya utani ya timu ya taifa ya Argentina: La Albiceleste (The Albiceleste), La Celeste y blanca (The White and Sky Blue)

Mfumo: Kikosi cha Argentina hutumia mfumo wa 3-4-3.

Image result for Lionel Messi (argentina)Mchezaji Nyota na nahodha: Lionel Messi (Barcelona)

Image result for Paulo Dybala (argentina)Mchezaji hatari: Paulo Dybala (Juventus).

Image result for Jorge Luis Sampaoli Moya (argentina)Kocha: Jorge Luis Sampaoli Moya (58), raia wa Argentina.

Ushiriki: Argentina imeshiriki fainali za kombe la dunia mara kumi na sita (16). Mwaka 1930, 1934, 1958, 1962, 1966, 1974, 1978, 1982, 1986, 1990, 1994, 1998, 2002, 2006, 2010 na 2014.

Mafanikio: kutwaa ubingwa (1978, 1986).

 

Kuelekea 2018:

Argentina ililazimika kusubiri mchezo wa mwisho wa kundi la Amerika ya Kusini ili kujihakikishia kucheza fainali za 2018.

Ilikuwa kama bahati kwao, kwani hali ilikuwa mbaya sana, na tayari ulimwengu wa soka ulifahamu mwaka 2018 Argentina wasingeweza kushiriki fainali hizo, huku wengine walidiriki kuandika katika mitandao ya kijamii “Fainali Za Kombe La Dunia Bila Messi.”

Kwa uzoefu na ujasiri wa wachezaji nguli wa Argentina Sergio Romero, Ángel Di María, Sergio Agüero, Gonzalo Higuaín, Lucas Biglia, Éver Banega na nahodha Lionel Messi walikata ngebe za waliowasema vibaya kwa kushinda mchezo wao wa mwisho dhidi ya Ecuador, jumla ya mabao matatu kwa moja.

Mchezo huo muhimu kwa argentina ulichezwa Estadio Olímpico Atahualpa, mjini Quito (Ecuador) Oktoba 10, 2017.

Mabao ya Argentina yalifungwa na Lionel Messi dakika ya 11′, 19′ na 62 huku bao la kufutia machozi kwa wenyeji likifungwa na Romario Andrés Ibarra Mina dakika ya kwanza.

Endapo ingetokea Argentina wanashindwa kufuzu fainali za kombe la dunia ingekuwa mara ya ya kwanza tangu mwaka 1958, ambapo walishiriki mfululizo hadi mwaka 2014 walipocheza mchezo wa hatua ya fainali dhidi ya Ujerumani na kufungwa bao moja kwa sifuri.

Taifa hili lenye watu zaidi ya 43,847,430 liliwahi kukosa fainali za kombe la dunia mwaka 1938, 1950, 1954 na 1970.

Kikosi cha Argentina kinakwenda nchini Urusi kikiwa na sifa ya safu bora ya ushambuliaji inayoongozwa na Lionel Messi, huku safu yao ya ulinzi ikitajwa kuwa bora kufuatia kuundwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa kama Gabriel Mercado, Javier Mascherano, Biglia, Enzo na Nicolás Otamendi.

Argentina wataanza kampeni za kuusaka ubingwa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Iceland, Uwanja Otkritie, mjini Moscow, Juni 16, kisha watapambana na Croatia Juni 21, Uwanja wa Nizhny Novgorod, mjini Nizhny Novgorod, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Nigeria Juni 26, Uwanja Krestovsky, mjini Saint Petersburg.

Ni Messi ndiye anayeangaliwa kwa jicho la tatu na mashabiki wote wa Argentina kuwa chachu ya kuivusha timu hiyo na kuamsha matumaini mapya kwa mashabiki wake.

Kama isemavyo kauli mbiu fulani, ni kweli yajayo yanafurahisha, tuendelee kutega masikio na macho yote nchini Urusi kuanzia katikati ya mwezi ujao. Dar24 inaendelea kumulika timu zote zitakazoshiriki fainali za kombe la dunia mwaka huu. Endelea kuwa hapa hapa na mwambie rafiki amwambie rafiki.

Kesho tutaimulika timu nyingine.

Dk. Saleh Ali Sheikh asifu amani na upendo wa Watanzania, "Ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine"
Kikao cha NEC champitisha Makongoro Nyerere, Mizengo Pinda