Hatua kwa hatua hadi Urusi, mwezi ujao kushuhudia mtanange utakaoamua nani atakuwa mbabe wa kulibeba Kombe la Dunia la Fifa mwaka huu. Dar24 inaendelea kumulika timu za kundi D, na leo tunaiweka kati Croatia.

Croatia iko na Argentina, Iceland, na Nigeria katika kundi hili, tayari tulishazimulika timu za Argentina na Iceland.

Ilifuzu fainali za kombe la dunia 2018, ikitokea ukanda wa barani Ulaya, (UEFA) baada ya kushika nafasi ya pili katika kundi la 9 (kundi I) lililokuwa na mataifa ya Iceland, Ukraine, Turkey, Finland na  Kosovo.

Croatia ilimaliza michezo ya kundi hilo kwa kufikisha alama 20, ikitanguliwa na Iceland waliokuwa kileleni kwa kujikusanyia alama 22.

Kanuni za kufuzu fainali za kombe la dunia ukanda wa barani Ulaya (UEFA) ziliibeba Croatia hadi kwenye mchezo wa mtoano, ambapo taifa hilo la Ulaya ya mashariki lilipangwa kupambana na Ugiriki.

Mchezo wa kwanza kwa wawili hao ulichezwa Stadion Maksimir, mjini Zagreb Novemba 9, 2017 na wenyeji walijitengenezea mazingira mazuri ya kufuzu, kwa kupata ushindi mabao manne kwa moja.

Mabao ya Croatia yalifungwa na Luca Modrić dakika ya 13 kwa mkwaju wa penati, Nikola Kalinić dakika ya 19, Ivan Perišić dakika ya 33 na Andrej Kramarić dakika ya 49, huku bao la Ugiriki likifungwa na Sokratis Papastathopoulos dakika ya 30.

Mchezo wa mkondo wa pili uliunguruma Karaiskakis Stadium, mjini Piraeus Novemba 12, 2017  ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.

Jina la utani la timu ya taifa ya Croatia: Vatreni (The Blazers)

Mfumo: Kikosi cha Croatia hutumia mfumo wa 4-2-3-1.

Image result for Luka Modric - croatiaMchezaji Nyota na nahodha: Luka Modric (Real Madrid)

Image result for Nikola Vlasic - croatiaMchezaji hatari: Nikola Vlasic (Everton).

Image result for Zlatko Dalić - croatiaKocha: Zlatko Dalić (51), raia wa Croatia.

Ushiriki: Croatia imeshiriki fainali za kombe la dunia mara nne (4). Mwaka 1998, 2002, 2006 na 2010

Mafanikio: Mshindi wa tatu (Mwaka 1998)

Kuelekea 2018:

Kocha Zlatko Dalic, alikuwa na kazi kubwa ya kufanya kutokana na uteuzi wake kufanywa siku kadhaa kabla ya kwenda katika mchezo wa mtoano dhidi ya Ugiriki.

Alionyesha kujiamini kwa kufanya uteuzi wa kikosi imara ambacho kilifanikiwa kupata tiketi ya kushiriki fainali za mwaka huu kwa kuifunga Ugiriki mabao manne kwa moja.

Kiungo na nahodha wa Croatia Luka Modric huenda fainali za mwaka huu zikawa za mwisho kwake kutokana na kuwa na umri wa miaka 32, lakini bado anategemewa sana kutokana na uwezo wake wa kumiliki sehemu ya kiungo.

Alikuwa muhimili mkubwa wakati Croatia ikisaka nafasi ya kushiriki fainali za 2018, na alifanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu.

Croatia wataanza kampeni za kuusaka ubingwa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Nigeria, Uwanja Kaliningrad, mjini Kaliningrad Juni 16, kisha watapambana na Argentina Juni 21, Uwanja wa Nizhny Novgorod, mjini Nizhny Novgorod, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Iceland Juni 26, Uwanja Rostov, mjini Rostov-on-Don.

Usikose kuitembelea YouTube Channel yetu ya Dar24 Media kupata mengi zaidi kuhusu Fainali za Kombe la Dunia, Burudani, Siasa na Maisha.

Thiago Silva: Hatuahidi ubingwa, tunaahidi soka la ushindani
Maajabu 7 ya korosho kwa mwili wa binadamu