Bado tunalimulika kundi A lenye timu zitakazochuana kuvuka hatua ya kwanza ya makundi kwenye Kombe la Dunia katikati ya mwezi ujao, na leo tunaimulika Saudi Arabia.

Saudi Arabia imefuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2018, ikitokea ukanda wa bara la Asia. Awali, walipangiwa kundi B wakati wa kuwania kufuzu fainali hizo sambamba na mataifa ya Japan, Australia, United Arab Emirates (UAE), Iraq na Thailand.

Saudi Arabia wenye idadi ya watu milioni 32.28 walimaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo, nyuma ya Japan na kufuzu moja kwa moja kuwania Kombe la Dunia kwenye fainali za mwaka huu.

Jina la utani: Green Falcons

Mfumo: 4-3-3

Mafanikio ya juu kwenye Kombe la Dunia: Hatua ya makundi.

 

Image result for Juan Antonio PizziKocha: Juan Antonio Pizzi (49), raia wa Argentina

Image result for Nawaf Al AbedMchezaji Nyota: Nawaf Al Abed wa klabu ya Al-Hilal.

Image result for Osama HawsawiNahodha: Osama Hawsawi. (Al-Ahli Saudi FC)

Image result for Fahad Al-MuwalladMchezaji Hatari: Fahad Al-Muwallad wa klabu ya Al-Ittihad.

 

Kuelekea 2018:

Haikuwa kazi rahisi kwa Saudi Arabia kufuzu fainali za kombe la dunia za 2018, kwani iliwalazimu viongozi wa shirikisho la soka nchini humo kubadilisha makocha mara kwa mara ili kufanikisha lengo hilo.

Miongoni mwa makocha waliopita kwenye timu hiyo na kufukuzwa ni Bert van Marwijk ambaye aliifikisha Uholanzi katika fainali ya michuano hiyo mwaka 2010 kule Afrika kusini.

Kuondoka kwa Van Marwijk kulitoa nafasi kwa viongozi wa shirikisho la soka la Saudi Arabia kumuajiri kocha kutoka Argentina Edgardo Bauza, ambaye alikiongoza kikosi cha Green Falcons kwa miezi miwili. Baadaye, mwaka 2016, aliajiriwa kocha Juan Antonio Pizzi, aliyekuwa amejiuzulu kuitumikia timu ya taifa ya Chile baada ya fainali za Marekani ya Kusini (Copa America) mwaka 2016.

Saudi Arabia haipewi nafasi kubwa ya kufanya vyema katika fainali za kombe la dunia, kutokana na kutokuwa na historia nzuri katika michuano hiyo tangu walipoanza kushiriki.

Taifa hilo kutoka barani Asia limeshiriki Fainali za Kombe la Dunia mara nne (4), mwaka 1994, 19982002 na 2006. Mara zote iliposhiriki haikuwahi kuvuka hatua ya makundi.

Saudi Arabia imepangwa katika kundi la kwanza sambamba na wenyeji wa fainali hizo Urusi. Wengine ni Misri na Uruguay.

Itaanza kampeni za kuusaka ubingwa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Urusi katika uwanja wa Luzhniki uliopo mjini Moscow Juni 14, kisha watapambana na Uruguay mjini Rostov-on-Don, kwenye uwanja wa Rostov Juni 20, na watamaliza michezo ya hatua ya makundi Juni 25 dhidi ya Misri, kwenye uwanja wa Volgograd, mjini Volgograd.

Kocha wa Saudi anakibarua cha kusafisha zaidi ‘CV’ yake kutokana na historia ya hivi karibuni ya kukinoa kikosi cha Chile kwenye Copa America mwaka 2016, lakini kilishindwa kutinga mashindao ya Kombe la Dunia.

Mpira ni dakika 90 na zile zitakazoongezwa yakitokea ya kutokea, huenda Saudi wakatunisha misuli na kuwakata ngebe za awali wenyeji Urusi, hakuna binadamu aijuaye kesho!

Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi fupi kila siku hapa Dar24, usisahau kutembelea YouTube Channel yetu ‘Dar24media’ upate historia ya matukio yaliyojiri kwenye kombe hili kupitia kipindi cha ‘Zaidi’.

Tunakusogeza karibu na Urusi hadi tushuhudie atakayebeba Kombe la FIFA. Kwa walioanza mfungo, ‘Ramadan Kareem’.

Mpitanjia agoma kujivua uwakili kesi ya Nondo
Bodi ya Mikopo yalalamikiwa kwa upendeleo