Tunafungua pazia la kundi G, kulimulika kuelekea fainaliza kombe la dunia. Na leo tunaanza na Ubelgiji yenye timu za Panama, Tunisia na Uingereza.
Ubelgiji ilifuzu fainali za kombe la dunia ikitokea ukanda wa barani Ulaya (UEFA), kwa kupambana na timu za mataifa ya Ugiriki, Bosnia & Herzegovina, Estonia, Cypras na Gilbrata zilizounda kundi H (Kundi La Nane).
Michezo ya kundi hilo ilishuhudia Ubelgiji walipambana kufa na kupona na mwishowe walifanikiwa kumaliza vinara kwa kushinda michezo tisa, huku wakitoka sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Ugiriki na hawakupoteza mchezo wowote.
Mwenendo huo mzuri uliwawezesha kufikisha alama 28 ambazo ziliwavusha moja kwa moja hadi katika fainali za kombe la dunia 2018.
Majina ya utani ya timu ya taifa ya Ubelgiji: De Rode Duivels, Les Diables Rouges na Die Roten Teufel (The Red Devils)
Mfumo: Kikosi cha Ubelgiji hutumia mfumo wa 3-4-2-1.
Mchezaji Nyota na nahodha: Eden Hazard (Chelsea)
Mchezaji hatari: Thomas Meunier (Paris St-Germain)
Kocha: Roberto Martínez Montoliu (44), raia wa Hispania.
Ushiriki: Ubelgiji imeshiriki fainali za kombe la dunia mara kumi na mbili (12). Mwaka 1930, 1934, 1938, 1954, 1970, 1982, 1986, 1990, 1994, 1998, 2002, na 2014.
Mafanikio: Mshindi wa nne (1986).
Kuelekea 2018:
Wakati wa michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka huu, Ubelgiji iliweka rekodi ya kufunga mabao 43 na mshambuliaji wao hatari anaeitumikia klabu ya Man Utd Romelu Lukaku aliweka rekodi ya kuwa mfungaji wa muda wote katika nchi hiyo.
Mpaka sasa Lukaku amefikisha mabao 33 akiifungia Ubelgiji, hali ambayo inatazamiwa huenda ikamuongezea morari ya kufanya vyema wakati wa fainali za kombe la dunia zitakazoanza rasmi Juni 14 nchini Urusi.
Kocha mkuu wa timu ya taifa la Ubelgiji lenye watu zaidi ya 11,358,357 Roberto Martínez, ana matumaini makubwa na kikosi chake, kutokana na uwepo wa wachezaji wenye uzoefu wa kupambana.
Baadhi ya wachezaji wa Ubelgiji ambao wanaaminiwa kufanya makubwa wakati wa fainali hizo ni Jan Vertonghen, Toby Alderweireld, Vincent Kompany na Kevin De Bruyne.
Kutokana na uwepo wa wachezjai wenye uzoefu, Ubelgiji ni moja ya mataifa yanayopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika fainali za mwaka huu, baada ya kushindwa kuonyesha machachari wakati wa fainali za mwaka 2014 nchini Brazil, kwa kuishia hatua ya robo fainali chini ya kocha Marc Wilmots.
Ubelgiji wataanza kampeni za kuusaka ubingwa wa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Panama, Uwanja wa Fisht Olympic mjini Sochi Juni 18, kisha watapambana na Tunisia Juni 23, Uwanja wa Otkritie mjini Moscow, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Uingereza, Juni 28, Kaliningrad mjini Kaliningrad.
Usikose na usiache kuendelea kufuatilia makala hizi, kesho tutaendelea kumulika timu za kundi hili. Nakukumbusha tena kuendelea kufuatilia channel yetu ya YouTube ya Dar24 Media.