Mashabiki watakaoshuhudia fainali za kombe la dunia 2018 na zile za kombe la mabara zitakazofanyika nchini Urusi baadae mwaka huu, watalazimika kuwa na vitambulisho maalum.
Wenyeji wa fainali hizo wamebaini mbinu hiyo, kwa kuhofia fujo ambazo huenda zikajitokeza baina ya mashabiki wa mataifa mawili ama matatu watakapokua ndani ama nje ya uwanja.
Urusi imechukua tahadhari hiyo, baada ya kujifunza mapungufu yaliyojitokeza wakati wa fainali za Ulaya (Euro 2016), ambapo mashabiki wa England na Urusi waliibua zogo jijini Paris.
Shirikisho la soka duniani FIFA limebariki mpango huo ambao utawawezesha watu wa usalama nchini Urusi kuwatambua kwa urahisi watu ambao watakua chanzo cha vurugu viwanjani kupitia vitambulisho hivyo.
Fainali za kombe la mabara zimepangwa kuanza mwezi Juni, na zitacheza katika viwanja vitakavyotumika wakati wa fainali za kombe la dunia mwakani.