Wanajeshi wa Urusi na Ukraine, wametupiana lawama wenyewe kwa wenyewe kwa kujiandaa kufanya shambulio la karibu kwenye kinu cha Nyuklia cha Zaporizhzhia nchini Ukraine, kitendo ambacho ni hatari na kinachowez kusababisha kutoka kwa mionzi.
Vikosi vya Urusi vinashikilia udhibiti wa kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, ambacho ni kituo kikubwa zaidi cha nguvu za nyuklia barani Ulaya tangu mwanzoni mwa mwezi Machi lakini wamewaweka wafanyikazi wa Ukrain mahala hapo ili kukiendesha.
Shirika la ujasusi la Ukraine limesema wahandisi walioajiriwa na Rosatom, kampuni ya nyuklia ya serikali ya Urusi, wameondoka kwenye kiwanda hicho na kwamba wafanyakazi wanaoendelea na majukumu yao pekee ndio watakaoruhusiwa kuwepo kwenye kiwanda hicho.
Kwa mara ya kwanza katika historia, vinu vya nyuklia viko katika eneo la vita, huku Waukraine wengi wakitambua hatari hiyo kuwa na athari kubwa kutokana na Kiwanda cha Chernobyl, kilichowahi kupata hitilifafu na kutokea ajali mbaya zaidi ya nyuklia duniani mwaka wa 1986 Ukrainia, kaskazini mwa mji mkuu wa Kyiv.
Jumba hilo la nyuklia limepata misukosuko kadhaa ya majibizano ya mashambulizi huku kila upande ukimlaumu mwingine na vikosi vya kijeshi vya Urusi vimechukua nafasi ndani na nje ya uwanja, na kusababisha mashtaka kuwa wanatumia Zaporizhzhia kama ngao, wakijua kwamba Waukraine watakosa cha kufanya.