Serikali ya Urusi imeahidi kushirikiana na Afrika kuboresha uchumi ikiwemo Tanzania inayoendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, kwa lengo la kuboresha uchumi na biashara kwa kutumia rasilimali zake ikiwemo madini, maliasili na kilimo.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya kumalizika kwa Mkutano wa pili wa kilele baina ya Wakuu wa nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi, uliofanyika kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum jijini St. Petersburg, Urusi.
Amesema, “mwelekeo wa mkutano ni kuona namna gani tunaweza kuboresha uchumi wa nchi za Afrika kwa pamoja na Urusi. Wametoa mwelekeo namna watakavyoweza kushirikiana na nchi za Afrika kuboresha uchumi wa kila nchi, na sisi tumeeleza mkakati wa kiuchumi kwenye nchi yetu ambao Rais Putin ameuridhia.”
Waziri Mkuu amesema Tanzania pia inasisitiza matumizi ya nishati mbadala kama njia muhimu ya kuwawezesha wananchi wa vijijini, ili nao wamudu kutumia eneo hilo kuinua uchumi wao na kukuza biashara ya mazao baina ya Afrika na Urusi.
Akifungua mkutano huo Rais wa Urusi, Vladmiri Putin alisema nchi za Afrika zimekuwa na mahusiano mazuri na ya muda mrefu na Taifa hilo na kwamba wanaendelea kutoa misaada bila vikwazo kwenye maeneo mbalimbali.