Urusi imelaani vikali hatua ya Marekani kumuunga mkono kiongozi wa upinzani wa Venezuela aliyejitangaza kuwa ndiye Rais wa mpito wakati Rais Nicolás Maduro akiwa madarakani.

Marekani ambayo ni hasimu wa Rais Maduro, jana ilitangaza kuwa inamtambua Juan Guaidó aliyejiapisha mwenyewe wakati maandamano makubwa ya kupinga Serikali yakiendelea.

Maelfu ya waandamanaji wanaopinga Serikali ya Rais Maduro

Urusi imesema kitendo hicho cha Marekani ni kutaka kupokonya madaraka halali ya Rais Maduro na kuchochea umwagaji damu. Imeeleza kuwa Marekani imevunja sheria za kimataifa kwa hatua iliyoichukua.

“Tunachukulia hatua ya kutaka kupokonya madaraka ya Serikali halali nchini Marekani kama hatua ya kutaka kuleta umwagaji damu na kuvunja sheria za kimataifa,” Reuters inaikariri taarifa ya Ikulu ya Urusi. “Tunamtambua Maduro kama kiongozi halali wa Serikali,” imeongeza.

Rais Maduro amewatimua wanadiplomasia wote wa Marekani nchini humo kama hatua ya kujibu mapigo na akatangaza kuvunja rasmi uhusiano na taifa hilo lenye nguvu duniani.

Mwanasiasa huyo anayeiongoza Venezuela tangu mwaka 2013, aliapishwa mapema mwezi huu kuongoza kwa muhula wa pili, baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi Mei mwaka jana. Ushindi huo umepingwa vikali na wapinzani wakidai kuwa ulitokana na wizi wa kura.

Guaidó ambaye ni kiongozi wa upinzani na kiongozi wa Bunge la Venezuela, amedai kuwa Katiba ya nchi hiyo inamruhusu yeye kama kiongozi wa Bunge kuiongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito ikiwa kuna hali ya sintofahamu ya matokeo ya uchaguzi.

Aliungwa mkono na Rais wa Marekani, Donald Trump aliyedai kuwa wanamtambua kama Rais wa mpito wa nchi hiyo, hatua ambayo imekosolewa vikali na jamii ya umoja wa mataifa.

Marekani pia imeyataka majeshi ya Venezuela kumuunga mkono Guaidó, lakini yamekataa na kubaki watiifu kwa Rais Maduro.

Marais wa Mexico, Bolivia, Cuba na Uturuki wameeleza kuwa wanamuunga mkono Maduro kuliongoza taifa hilo lenye watu milioni 32 na utajiri wa mafuta.

“Ndugu yangu Maduro kuwa imara, tunasimama nawe,” ametweet Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan.

Maduro alipokea kijiti cha kuiongoza Venezuela kutoka kwa Hugo Chavez aliyekuwa Rais wa nchi hiyo wakati yeye akiwa Makamu wake.

Rais mpya wa DRC augua ghafla baada ya kuapishwa
Kizimbani kwa kuchapisha uongo dhidi ya Rais Magufuli