Urusi inaripotiwa kuzidisha mashambulizi yake kwenye miji kadhaa nchini Ukraine usiku wa kuamkia leo.
Kwa mujibu wa jeshi la Ukraine, limekabiliana vikali na vikosi vya Urusi kwenye ukingo wa mji wa kusini wa Mykolayiv, ambao uko njiani kuelekea bandari kubwa kabisa ya Odessa.
Taarifa zinaongeza kwamba raia kadhaa wameuawa kwenye mapigano ya kuwania udhibiti wa mji wa Chernihiv ulio upande wa kaskazini.
Rais Volodymr Zelensky amesema pia kwamba makombora ya Urusi yameuharibu uwanja wa ndege wa Vinnytsia ulio katikati mwa Ukraine.
Haya yanajiri huku makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda ili kupisha operesheni za kibinaadamu yakivunjwa kwa mara ya pili mfululizo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, raia waliouawa tangu uvamizi wa Urusi uanze ni 364, wakiwemo watoto 20, huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.