Baada ya kuitumikia timu ya taifa ya Hispania katika michezo 131 na kutwaa mataji matatu makubwa dunaini, kiungo aliyetamba na FC Barcelona kuanzia mwaka 2002 hadi 2018 Andrés Iniesta Luján, ametangaza kustaafu soka la kimataifa.
Iniesta amechukua maamuzi hayo, baada ya kikosi cha Hispania kuondolewa kwenye fainali za kombe la dunia hatua ya 16 bora, kwa kufungwa na wenyeji Urusi, kwa changamoto ya mikwaju ya penati jana jumapili.
Hata hivyo maamuzi hayo yalitarajiwa, kufuatia kiungo huyo kuwahi kusema katika vyombo vya habari kuwa, endapo Hispania itaondolewa kwenye fainali hizo, zinazoendelea nchini Urusi, atachukua maamuzi ya kustaafu soka la kimataifa.
“Ulikua mchezo wangu wa mwisho kuitumikia Hispania, ninaamini nimeitumikia timu hii kwa moyo wote tangu mwaka 2006 nilipoitwa kwa mara ya kwanza,” alisema Iniesta kuwaambia waandishi wa habari.
“Wakati mwingine huna budi kukubaliana na matokeo, binafsi nimekubali tumepoteza na imekua mwisho wangu kuitumikia Hispania kwa upande wa timu ya taifa.”
Iniesta anaondoka kwenye timu hiyo huku akikumbukwa na mashabiki wengi wa soka duniani, kufuatia bao lake la ushindi dhidi ya Uholanzi mwaka 2010 nchini Afrika kusini, ambalo liliipa ubingwa wa kwanza wa dunia Hispania.
Mbali na mafanikio hayo, Iniesta pia alikua miongoni mwa wachezaji wa Hispania waliotwaa mara mbili mfululizo ubingwa wa Ulaya mwaka 2008 na 2012.
Maamuzi ya kustaafu soka la kimataifa pia yanaendana na hatua ya kuondoka FC Barcelona mwishoni mwa msimu uliopita, huku akitarajia kuanza maisha mapya akiwa na klabu ya Vissel Kobe inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Japan.