Majeshi ya Urusi yameisambaratisha ngome muhimu ya Ukraine na kudhibiti Jiji la Severodonetsk, ambalo ni kitovu cha mapigano makali zaidi Mashariki mwa Kanda ya Donbas.

Kwa mujibu wa Aljazeera, mapigano makali ya ‘mtaa kwa mtaa’ yameshuhudiwa Wikendi iliyopita na kwamba Urusi inadhibiti zaidi ya asilimia 70 ya jiji hilo.

Gavana wa Luhansk, Serhiy Haidai amesema majeshi ya Urusi yanapata ushindi kwa kasi yakishambulia nyumba kwa nyumba, hali inayowalazimisha wanajeshi wa Ukraine kurudi nyuma na kujikusanya upya.

“Kwa bahati mbaya, maadui wanaharibu kirahisi majengo yaliyokuwa yanatumika kama maficho yetu. Kwa hatua hii, ni vigumu sana kwa sababu maadui wanafunga mitaa, wakimaliza wataanza kupiga makombora kila nyumba ya jirani,” Gavana Haidai  amekaririwa.

Naye Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amewasifu wapiganaji wa nchi hiyo walio katika jimbo la mapigano akieleza kuwa anajivunia sana jinsi wanavyomkabili adui.

Moshi unaofuka katika jiji la Severodonetsk baada ya kushambuliwa na Urusi

Rais Zelensky ameeleza kuwa Severodonetsk ndilo eneo la mapambano makali zaidi katika mkoa wa Donbas na kukiri kuwa wanapata wakati mgumu.

“Severodonetsk inabaki kuwa kitovu cha mapambano makali zaidi katika eneo la Donbas. Haya ni mapambano makali zaidi, huenda ni moja kati ya mapambano magumu zaidi tangu vita ilipoanza,” amesema Rais Zelensky.

Severodonetsk ni eneo muhimu zaidi kwenye Mkoa wa Donbas lenye viwanda vingi vya kimkakati, Mashariki mwa Ukraine. Eneo hilo limekuwa likishuhudia mapigano tangu mwaka 2014 ambapo makundi ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi walifanikiwa kudhibiti baadhi ya maeneo na kujitangazia Jamhuri ya Watu wa Donetsk na Jamhuri ya Watu wa Luhansk.

Aliyetoka gerezani kwa huruma ya Rais amkata mapanga mama yake
EU yataka demokrasia na amani Zanzibar