Majeshi ya Urusi yameanza tena kukishambulia kiwanda cha chuma cha Azovstal ambapo ndiyo sehemu ya mwisho walipo wanajeshi wa Ukraine mjini Mariupol baada ya mji huo kushambuliwa kwa mfululizo wa mabomu tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake mnamo Februari 24.
Mashambulizi katika kiwanda hicho yalikuwa ni sehemu ya msururu wa mashambulizi yaliyofanywa jana kote nchini Ukraine ambapo serikali inasema watu 21 wameuwawa katika eneo la Donetsk mashariki mwa nchi hiyo.
Urusi inakishambulia kiwanda cha Azovstal kwa magari ya kivita na vifaru huku Rais Volodymyr Zelenskiy akisema mashambulizi ya sasa ya Urusi yanaonyesha wazi kwamba Urusi haina lengo la kijeshi.
Umoja wa Mataifa umesema watu 101 wameokolewa kutoka kwenye mahandaki ya enzi za muungano wa Sovieti chini ya kiwanda hicho cha chuma cha Azovstal kama sehemu ya operesheni ya siku tano.
Haya yanafanyika wakati Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya umependekeza vikwazo vipya kwa mafuta ya Urusi kutokana na uvamizi huo wa Ukraine.